Na Alex Siriyako,
Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tabora imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw.Hassani Wakasuvi ambae aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dr. Batilda Burian pamoja na wajumbe wengine wa kamati wakiwemo; Maimuna Abbas, Lukas Sereli, Imani Matabula pamoja na Mwashamu Hashimu ambaye ni mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora.
Vilevile Kamati hii iliambatana na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Tabora ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Mohamedi Katete, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahaya Nawanda, Meya wa Manispaa ya Tabora Mh. Ramadhani Kapera , Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bw. Seif Salum Seif, Wajumbe wa kamati pamoja na wataalamu wa Idara mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Kamati hii imetembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika Manispaa ya Tabora ikiwa ni miradi inayotekelezwa kwa fedha kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Mapato ya ndani ya Halmashauri, Fedha za tozo za Miamala ya simu, Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 pamoja na fedha za maendeleo kutoka Serikali kuu.
Miongoni mwa miradi iliyopata fursa ya kutembelewa na kukaguliwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ni pamoja na Madarasa matano na Ofisi moja (Milioni mia moja kutoka mradi wa UVIKO-19), Umaliziaji wa Madarasa matatu na Ofisi moja (Milioni 25, fedha za TOZO), Ukamilishaji wa Maabara moja ya Sayansi (Milioni 30, Fedha kutoka Serikali Kuu), Miradi yote hii imetekelezwa katika Shule ya Sekondari Ipuli, Kata ya Ipuli. Kamati imekagua Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora (Fedha za Maendeleo kutoka Serikali Kuu), ambapo kuna majengo mengi yanayoendelea kujengwa kama jengo la Utawala, Jengo la Mama na Mtoto, Maabara,na OPD. Jengo la Huduma kwa Wagonjwa wa Nje(OPD) limekamilika na huduma zinatarajia kuanza kutolewa Janauri 15,2022.
Kamati imekagua vilevila ujenzi wa madarasa matatu na Ofisi moja Shule ya Msingi Kakola, Kata ya Kakora (Zaidi ya milioni 23, Mapato ya ndani) ambapo ujenzi uko hatua za umaliziaji. Kamati imekagua Madarasa mawili na Ofisi Shule Shikizi ya Tumbi, Kata ya Misha (Milioni arobaini, UVIKO-19),= na Kamati imemaliza Ziara yake kwa kukagua Ujenzi wa Kituo cha Afya Misha (Milioni 250, fedha za TOZO) ambapo kwa awamu ya kwanza yanajengwa majengo matatu, Jengo la Huduma kwa Wagonjwa wa nje(OPD), Maabara na kichomea taka. Ujenzi wa mradi huu uko hatua ya kupandisha boma.
Mwenyeki wa Kamati Bw. Hassani Wakasuvi kwa niaba ya Kamati kwanza aliridhika na ubora na gharama za miradi pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za dhati kabisa za kuwaletea maendeleo Watanzania hususani wakazi wa Manispaa ya Tabora kwa kuwapatia kiwango kikubwa cha fedha na kwa muda mchache sana kwenye miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu, Afya, Maji na Barabara. Vilevile amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahaya Nawanda , Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Bw. Mohamedi Katete, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mh. Ramadhani Kapela pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bw.Seif Salum Seif kwa umoja wao wa kuunganisha nguvu na kuwa kitu kimoja katika usimamizi wa miradi hii ya maendeleo.
Bw. Hassani Wakasuvi pamoja na kuridhika na ubora wa miradi na namna fedha ilivyosimamiwa vizuri, alitoa maelekezo kwa Watendaji hususani Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, miongoni mwa maelekezo ni kujenga uzio kuzunguka shule ya Sekondari Ipuli, Kuweka mpango wa kujenga uzio kuzunguka Hospitali ya Wilaya, Kuweka mipango ya Kibajeti ya kujenga nyumba za Watumishi katika Hospitali ya Wilaya na Kituo cha Afya Misha pamoja na Halmashauri kujipanga kuanza kufikiria kujenga madarasa ya ghorofa kwani ardhi haiongezeki na mji unakuwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora nae amempongeza Mama Samia Suruhu Hassan kwa moyo wake wa huruma na upendo kwa Watanzania hususani kwa Wakazi wa Wilaya ya Tabora kwani ameleta fedha nyingi sana za maendeleo ngazi ya Kata, Fedha ambazo pamoja na Ujenzi wa miradi lakini pia zimekuwa fursa kubwa kwa ajira kwa vijana wa Tabora na Wajasiriamali wengine. Vilevile amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tabora na kuahidi kusimamia maelekezo na ushauri walioutoa kwa ustawi wa Manispaa yetu na Mkoa wa Tabora kwa ujumla
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.