Na Alex Siriyako
Kamati ya Siasa ya Chama cha Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora leo imefanya ziara ya kutembelea na kukagua Miradi ya Maendeleo saba iliyopo hapa Tabora Manispaa na kuridhishwa nayo.
Akizungumza kwenye kikao cha majumuisho ya ziara Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mhe. Mohamed Katete alisema kuwa, chama kimeridhishwa sana kwa namna ambavyo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inavyotekeleza Miradi hiyo.
Katete alisema kuwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo unaleta faraja sana jambo ambalo wao kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na ndiyo wenye Ilani ya Chama ambacho kinaongoza Nchi wameona lina akisi na kwenenda na matarajio ya Chama katika kuisimamia Serikali.
“Sisi kama Chama kinachosimamia Serikali katika Ilani yetu tuliahidi mambo kadha wa kadha na hapa tumeona mnayatekeleza, hivyo tumeridhishwa sana na kwamba mnakwenda sambamba na matakwa ya Chama, hongereni sana kwa hili”, alisema Katete.
Siku ya kwanza Kamati ilitembelea na kukagua miradi minne ikiwa ni Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Itulu Kata ya Ndevelwa wenye thamani ya zaidi ya Milioni 50 ambapo ujenzi wake unaendelea na umefikia hatua ya umaliziaji, ikafuatiwa na ukarabati wa majengo kwenye Shule ya Sekondari Tabora Wavula wenye thamani ya Milioni 500 fedha kutoka Serikali Kuu na kwamba ukarabati huo umekemilika.
Kamati pia iliendelea na ukaguzi kwenye mradi wa ujenzi wa Madarasa mawili (2) pamoja na matundu ya vyoo 12 Shule ya Sekondari Kanyenye iliyopo Kata ya Malolo vikiwa na thamani ya zaidi ya Milioni 50, ambapo ipo hatua ya upauaji, na baadae Kmati ya Siasa ilitembelea na kukagua ujenzi wa Madarasa 2 pamoja na matundu ya vyoo 12 kwenye Shule ya Msingi Mwinyi ikiwa na thamani ya zaidi ya Milioni 50 ambapo ipo kwenye hatua ya Boma.
Siku ya pili Kamati ilipata wasaa wa kutembelea na kukagua miradi mingine mitatu ambapo ilianza kwa kukagua ujenzi wa Zahanati ya Ikomwa ambao utagaharimu zaidi ya Milioni 70 ikiwamo na nguvu za wananchi, ikafuatiwa na ukaguzi wa ujenzi wa Zahanati ya Misha iliyopo Kata ya Misha wenye thamani ya zaidi ya Milioni 50 na kwamba ujenzi kwa Zahanati zote mbili ujenzi badoo unaendele.
Kisha Kamati iliendelea na ukaguzi kwa Kituo cha Afya Tumbi kilichopo Kata ya Tumbi, mradi ambao umegharimu zaidi ya Milioni 200 kimekamilika na kinatoa huduma tayari, na baadae kamati ilihitimisha ziara yake kwa kukagua Vikundi 4 vya Ujasiliamali kati ya hivyo vikundi 2 vimepata mkopo hivi karibuni na vingine 2 vilikwisha pata siku nyingi na vipo kwenye marejesho vikiwa na jumla ya Milioni 35.
Wakitoa maoni wajumbe wa Kamati ya Siasa walisema wameridhishwa sana kwa namna ambavyo Serikali ya Wilaya ya Tabora inavyotekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo, na kwa kauli moja wajumbe wa kamati walimpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu pamoja na Wizara zinazohusika katika miradi hiyo kwa namna ambavyo wameamua kutatua kero nyingi zinazowakabili wananchi hasa wa Wilaya ya Tabora.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mheshimiwa Dkt. Yahya Ismail Nawanda aliwashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Siasa Wilaya kwa namna ambavyo wameweza kutembelea, kukagua, kushauri na kupongeza kwa miradi yote waliyopita. Na kwamba wao kama Serikali ya Wilaya wamepokea yote na kwamba ushauri wao wameupokea na kwamba wataufanyia kazi na kurekebisha penye kasoro.
Ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora ina lengo la kuwawezesha wajumbe wa Chama waweze kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, kushauri na kupongeza inapobidi kwa minajiri ya kuboresha na kuisadia Serikali kwenye utekelezaji wa Ilani inayolenga kuwaondolea kero wananchi na kuwasogezea huduma karibu kama ilivyo dhamira njema ya Mhe. Rais na Chama pia.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.