Na Alex Siriyako;
Kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Mwenyekiti wa kamati hii Mheshimiwa Razaro Nyamoga ametoa shukrani za dhati kwa Mheshiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule wanafunzi wa Kata za Kakola na Mtendeni, kwani sasa wanafunzi hawa wanasomea katika shule zao mpya kabisa ambazo zimejengwa karibu kabisa na makazi yao.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI leo Agosti 6, 2024 imefanya ziara ya kukagua miradi katika Manispaa ya Tabora, ikiwa ni mwendelezo wa zaira yao Mkoani Tabora, ambapo wamekagua shule za Kakola Sekondari iliyopo Kata ya Kakola, pamoja na Shule ya Msingi Kidatu iliyopo Kata ya Mtendeni.
Shule ya Sekondari Kakola kukamilika kwake kumewaondolea adha wanafunzi wa Kata ya Kakola ambao walikuwa wanalazimika kusomea Shule ya Sekondari Misha, iliyopo Kata ya Misha Pamoja na Shule ya Sekondari Nkumba iliyopo Kata ya Uyui, na kulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa kumi na tano kila siku.
Shule ya Msingi Kidatu imewaondolea adha ya kulundikana katika Shule ya Msingi Magereza iliyopo Kata ya Mtendeni, hivyo kuwapa fursa ya kusomea mazingira mazuri pasi na kubanana, lakini vile vile kulingana na ukubwa wa Kata hiyo ya Mtendeni, wanafunzi hawa hutumua muda mchache kwa sasa kufika shule hii mpya ya Kidatu.
Aidha, Mheshimiwa Nyamoga amewasihi sana wazazi wawahimize watoto kusoma shule kwa bidii na wasiwakatize masomo yao kwa sababu yeyote ikiwamo kuwaozesha na kuwapeleka watoto kuchunga mifugo wakati wa masomo.
Amesisitiza sana ujumbe huu kwa kuzingatia kuwa, miongoni mwa changamoto zinazoikabili Manispaa ya Tabora ni pamoja na wanafunzi wengi hasa wa elimu ya Sekondari katika Kata za pembezoni mwa Manispaa hii ambazo zilikuwa bado hazijapata shule za sekondari kutokumaliza masomo yao, na sababu kubwa ikitajwa kuwa ni umbali mrefu kwenda shule, changamoto ambayo kwa sasa imetatuliwa.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Manispaa Tabora, 4 Barabara ya Kiwanja cha Ndege
Anwani ya Posta: S.L.P 174, 45182 Tabora
Simu ya Ofisi: +255 262606088
Simu ya Mkononi: +255
Barua Pepe: md@taboramc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.