Na Alex Siriyako;
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeipongeza Manispaa ya Tabora kwa utoaji wa Mikopo ya asilimia kumi (10%) kikamilifu na yenye tija kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kupitia asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Aidha kamati imeipongeza Manispaa ya Tabora kwa ujenzi wa miradi mizuri kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha.
Haya yameelezwa leo tarehe 17 Machi 2023 wakati kamati hii ambayo imeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Stanslaus Mabula (Mb), ambae ameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt.Festo Dugange, kukagua miradi ya maendeleo pamoja na miradi ya vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia kumi.
Kamati imekagua Kituo cha Afya cha Tumbi, Ukarabati wa Bweni pamoja na ujenzi wa Viwanja vya Michezo Shule ya Tabora Wavulana, Kikundi cha Vijana cha Miombo Bee Keepers Initiative Group ambacho kinafuga nyuki pamoja na kusindika mazao ya nyuki kwa kuyaongezea thamani, pamoja na Kikundi cha Wanawake cha Holy Kitchen ambacho kinapika chakula (Catering), kinaoka keki, pamoja na kusindika Maziwa ya Ng’ombe.
Wajumbe wa Kamati kwa ujumla wameridhika na ubora wa majengo ya Kituo cha Afya Tumbi kwani ujenzi ulifuata BOQ na thamani ya fedha zilizoletwa na Serikali takribani milioni 500 zinaonekana. Hata hivyo, Mwenyekiti na Wajumbe wameiagiza mamlaka ya maji safi na salama Mkoani Tabora (TUWASA) kuharakisha upatikanaji wa maji safi ,salama na yenye uhakika kituoni hapo.
Wajumbe wa kamati wamekagua ukarabati wa bweni shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana, ukarabati uliogharimu Zaidi ya milioni 500 ambapo wameridhika na ukarabati huo japo wameitaka Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI kuona umuhimu wa kutafuta fedha na kuzikarabati shule zote kongwe za Mkoa wa Tabora kwani hali ya miundombinu ya shule hizi haiendani na ukubwa wa majina ya shule hizi.Vilevile wajumbe wamekagua mwenendo wa ujenzi wa viwanja vipya vya michezo vinavyojengwa shule ya Tabora Wavulana kwa gharama ya takribani milioni 540, viwanja ambayo vinatarajia kuongeza ufanisi katika michuano ya UMITASHUMITA NA UMISETA , michezo ambayo ilifanyika mwaka jana na inatarajia kufanyika Manispaa ya Tabora tena mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali itaendelea kuzisimamia Halmashauri na kuhakikisha zinafanya vizuri zaidi kwenye mikopo ya asilimia kumi, na kwa suala la ukarabati wa shule kongwe, kwa niaba ya TAMISEMI, amelichukua na kuahidi kwenda kulifanyia kazi.
Bi. Irene Malle, Mwenyekiti wa Kikundi cha Holy Kitchen, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan kwa mkopo wa milioni hamsini kwenye kikundi hicho, na ameahidi kufanya vizuri Zaidi na kurejesha mkopo huo kwa wakati.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.