Na Alex Siriyako,
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Ndugu Ramadhani Kapela, ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Fedha na Utawala, akiongozana na wajumbe wa kamati hiyo wa baraza la Madiwani, akiambatana vilevile na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora,Ndugu Sefu Salum, Katibu Tawala wa Manispaa ya Tabora,Ndugu Hamarskjold Yonaza, pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo, ameiongoza kamati hiyo kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Kamati ya fedha ikiwa ni miongoni mwa kamati mbalimbali za Baraza la Madiwani, imefanya ziara ya siku mbili mfululizo kuanzia tarehe 12/08/2021 hadi leo hii tarehe 13/08/2021, ambapo kimsingi imefanya ziara hii kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Katika Sekta ya elimu, miradi iliyotembelewa na kukaguliwa katika ziara hii ni pamoja na Ujenzi wa matundu kumi na mawili katika shule ya msingi Igombe B, na ujenzi unaendelea vizuri. Aidha kamati ilikagua vyumba vya madarasa viwili na ofisi ya walimu katika sekondari ya Ipuli, kata ya Ipuli, Kamati ilikagua vilevile vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu , matundu kumi na mawili ya vyoo katika shule ya Msingi Majengo kata ya Mpela.
Katika sekta ya Afya, Kamati ilikagua Hospitali ya Wilaya ya Tabora ambayo ujenzi wake unatekelezwa kwa nguvu ya serikali kuu pamoja na nguvu ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Ujenzi unaendelea na Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD),Kichomea taka(incinerator), na Maabara yako kwenye hatua za umaliziaji. Huduma kwa wagonjwa wa nje zinatazamiwa kuanza hivi karibuni. Vilevile jengo la Mionzi(Radiology), Jengo la mama na motto (Maternity Ward), Jengo la kufulia nguo( Laundry), Jengo la Utawala na Stoo ya dawa ni miongoni mwa majengo yanayoendelea kujengwa.
Kamati ilipata kukagua umaliziaji wa Zahanati ya Itulu, ambayo inajengwa kwa nguvu za Serikali kuu, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na nguvu za Wananchi wa kijiji cha Itulu. Zahanati hii inatazamiwa kugharimu zaidi ya milioni sabini mpaka kukamilika.
Zahanati ya Igombe ni miongoni mwa miradi iliyokaguliwa, zahanati hii inajengwa kwa nguvu kubwa ya pesa kutoka Serikali kuu pamoja na nguvu ya wadau wa maendeleo na Wananchi wa kijiji cha Igombe. Utekelezaji wa mradi huu unatizamiwa kugharimu zaidi ya milioni sabini kwa mujibu wa tathimini ya kamati ya ujenzi. Kamati vilevile iliweza kukagua umaliziaji wa Zahanati ya Igosha, Zahanati ya Igosha inajengwa kwa nguvu kubwa kutoka serikali kuu, Nguvu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na nguvu za wananchi wa kijiji cha Igosha na mradi uko hatua za umaliziaji.
Kamati ilipata wasaa wa kukagua kikundi cha wajasiriamali cha SHANI YA MUNGU kilichopo kata ya Gongoni kikiwa ni miongoni mwa vikundi vinavyonufaika na mikopo itolewayo na Halmashauri na kimepata mkopo wa shilingi milioni tano. Hiki ni kikundi cha wanawake wajasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji wa kuku, na vilevile kila mwanakikundi anakazi zake kama kuuza mkaa, kupika keki, kuuza nguo na kadhalika.
Katika majumuisho, wajumbe wa kamati walitoa maagizo kwa Wakuu wa Idara na Vitengo husika kufuatilia kwa umakini na kwa ukaribu zaidi ujenzi wa miradi kwani walibaini changamoto zinazojitokeza kati ya kamati ya ujenzi moja na nyingine, hivyo baadhi ya kamati zinahitaji kujengewa uwezo ili zifanye kazi kwa weledi na ufanisi zaidi na kuokoa fedha zaidi kama ilivyo malengo na madhumuni ya Serikali ya kutumia mfumo wa Force Account.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.