Na Alex Siriyako:
Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imeipongeza Menejimenti ya Manispaa kwa usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika katika Kata mbalimbali za Manispaa hii.
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Fedha na Utawala wametoa pongezi hizi leo Mei 3, 2023 katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo,ziara ambayo imefanyika kwa siku mbili mfululizo kwa maana ya tarehe mbili hadi tatu, Mei ,2023.
Kamati imeweza kukagua ujenzi wa Jengo jipya la Utawala la Manispaa ya Tabora, Ujenzi wa majengo manne ambayo ni Wodi ya Wanaume, Wodi ya Wanawake, Wodi ya Watoto pamoja na Mochwari katika Hospitali ya Wilaya, Vyumba Viwili vya Madarasa na Ofisi moja katika Shule ya Msingi Bombamzinga , Kata ya Isevya, Ujenzi wa Zahanati ya Ng’ambo, Kata ya Kidongo Chekundu pamoja na Ujenzi wa Viwanja vya Mpira wa Miguu, mpira wa wavu, mpira wa kikapu katika Shule ya Tabora Wavulana, viwanja vinavyotarajiwa kutumika katika michezo ya UMISSETA na UMITASHUMITA mwaka huu kuanzia tarehe mbili, Juni.
Mhe. Nassir Mnenge, Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora, kwa niaba ya wajumbe amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia Manispaa ya Tabora fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo na kuongeza kuwa Baraza la Madiwani kupitia Kamati zake za Kudumu litafanya kazi zake ipasavyo kuhakikisha kuwa miradi inajengwa kwa ubora uliuokusudiwa na thamani ya fedha katika miradi inaonekana.
Aidha pamoja na kuridhishwa na ubora wa majengo na thamani ya fedha iliyotumika, Wajumbe wameazimia fundi anayejenga Zahanati ya Ng’ambo iliyopo Kata ya Kidongio Chekundu asimamiwe kurekebisha makosa yaliyobainishwa na pindi akimaliza kurekebisha makosa hayo mkataba wake usitishwe mara moja kwani amekuwa mlevi wa kupindukia na kushindwa kumudu vema majukumu yake.
Katika kuhitimisha Ziara hii, Mhe. Nassir amewasihi sana Wataalamu wa Manispaa ya Tabora kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na wajenge utamaduni wa kukubali kukosolewa na kupokea ushauri wa wadau mbalimbali hususani kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.