Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kutoa kiasi cha Milioni Tano fedha za kitanzania kwa kila Kata ambapo zitaenda kusaidia urekebishaji wa miundombinu ya barabara.
Hayo yalisemawa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru alipokuwa akitoa ufafanuzi wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
‘’Halmashauri ya Manispaa imetenga kiasi cha Milioni Tano (5) kwa kila Kata pesa ambazo zitaletwa kwenye Kata zenu kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu hasa ya barabara, ambapo sasa kila Kata itaangalia vipaumbele kulingana na jiografia ya Kta yenyewe na viunga vyake ione kwamba ianze na barabra ipi angalau kuikwangua ili iweze kupitika au kuboresha mitaro kutegemea na ukubwa wa tatizo lenyewe,’’ alieleza Mkurugenzi Ndunguru.
Katika hatua nyingine Diwani wa Kata ya Mwinyi Mhe, Martin Daniel alimueleza Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani kuwa Tarura Manispaa wanapaswa kuitazama Kata ya Mwinyi kwa jicho la tatu kwa kuwa jiografia yake ilivyo inapokea maji mengi sana yanayotiririka kutoka sehemu tofauti tofauti kama vile Ng’ambo, Kanyenye na kadharika.
Aidha Mhe, Martin alimuomba Mwenyekiti ili Baraza la Madiwani liwaombe Tarura waiangazie pia Kata ya Mpera ambayo pia imekuwa ikiathiriwa sana hasa pale ambapo mvua inakuwa imenyesha, kwa kuwa miundombinu yake haimudu wingi wa maji hivyo kupelekea maji kujaa barabarani na kwenye makazi ya wananchi. Tatizo hilo hupelekea hata watoto washule kushindwa kwenda shule na kuhatarisha maisha ya wakazi wanaoishi maeneo hayo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ikomwa Mhe, Salum Msamazi aliwapongeza sana Tarura kwa namna ambavyo wamekuwa wakitekeleza na kushughurikia kazi zao na matatizo ya kimiundombinu ya barabara, jambo ambalo hupelekea kuondoa kero wanazokabiliana nazo wananchi hasa wa Kata ya Ikomwa.
‘’Kwa upande wangu nawapongeza sana Tarura kwa namna ambavyo wamaekuwa wakishughurikia matatizo yanayowakuta wananchi hasa wa kata yangu kwenye suala zima la miundombinu, hata ukiwapigia simu Tarura wanafika kwa haraka na wanatatua tatizo husika kwa kweli napongeza sana, pia nampongeza zaidi Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora pamoja na Menejimenti yote kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na uongozi wa Kata ya Ikomwa,’’ alisema Mhe Msamazi.
Naye Meneja wa Tarura Tabora Manispaa Mhandisi Edwin Kabwoto aliwaeleza wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Madiwani kuwa, amepokea michango na maoni yote kutoka kwa wajumbe na kwamba naichukua na kwenda kuifanyia kazi. Aliongeza kusema kwamba Tarura Manispaa inafanya kazi kwa weredi na uwazi mkubwa sana na bila upendeleo wa Kata yoyote ile , aidha alisisitiza kuwa atakuwa akiwasilisha mpango kazi wa Tarura kwenye kila Mkutano wa Baraza ili kuweka uwazi zaidi na mwisho aliwaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa Waheshimi wa Madiwani wote, Menejimenti ya Manispaa pamoja na wadau mbalimbali ili kuifanya Tarura kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na hatimaye kuifanya Tabora Manispaa kuwa sehemu bora na ya mfano zaidi kwa miundombinu.
Mkutano wa pili wa Baraza la Madiwani Tabora Manispaa ulifanyika kwa siku mbili ulimalizika kwa wajumbe wote kupokea taarifa mbalimbali kutoka kwenye Kamati za Kudumu na kutoka kwenye kila Kata
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.