Na Alex Siriyako,
Agosti 3,2021 imekuwa siku ya kihistoria katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ni baada ya kupokea chanjo za Uviko-19 za awamu ya kwanza. Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ni miongoni mwa halmashuri saba zinazounda Mkoa wa Tabora ambapo zote hizi zimepata mgao huo wa chanjo,huku wilaya ya Tabora ikipata chanjo 4030.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt.Baraka Msumi amefafanua kuwa Wilaya ya Tabora imepata dozi za chanjo 4030 kwa awamu hii ya kwanza, na kipaumbele kwa sasa ni Watu wenye umri zaidi ya miaka hamsin(50), wenye magonjwa sugu na watumishi wa Idara ya Afya. Na akafafanua zaidi kwamba vituo vya chanjo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuwa ni Hospitali ya Rufaa Kitete, Kituo cha afya Maili Tano,kilichopo Ipuli, pamoja na Zahanati ya Town Clinic.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt.Yahaya Nyawanda, wakati akiwaongoza wakazi wa Tabora kupata chanjo hizo, amemshukuru Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suruhu Hassani kwa kutupatia chanzo hizi 4030 watu wa Wilaya ya Tabora. Dkt.Nyawanda pia amewasihi wakazi wa wilaya ya Tabora kuja kupata chanjo hizi kwani ni tunu na fursa kubwa kwa wakazi wa Tabora manispaa. Amesisitiza kwamba chanjo ni bure na ni za hiari kwa wanaohitaji hususani wale wiliotajwa katika makundi yaliyopewa kipaumbele.
Katibu Tawala wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Ndugu Hamarksjold E.Yonaza ,nae alikuwa miongoni mwa watu wachache waliopata fursa ya kupata chanjo hii kwa siku ya leo, na aliweza kutoa nasaha zake kwa wakazi wa Tabora, amefafanua kuwa chanzo zimekuwepo sana, watu wamechanja chanjo za Polio, ndui na kadhalika. Amewasihi wakazi wa Tabora kujitokeza kwa wingi kuja kupata chanjo hii kwani ni bahati kubwa kuipata , kwamba kuna Watanzania wamesafiri kwenda mpaka nje ya nchi hii kufuata chanjo hii ya UVIKO-19.
Hali kadhalika, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Ndugu Sefu Salumu, nae alibahatika kuwa miongoni wa watu wachache waliopata fusa ya kupata chanjo hii kwa siku ya leo. Ndugu Sefu amewaasa wakazi wa Tabora kuachana na maneno ya mtaani na badala yake wawaone wataalamu wa Afya mahala popote pale wapate majibu sahihi juu ya chanjo hizi kwani kuna taarifa nyingi mtaani zisizo za kitaalam na wakazi wa Tabora wazipuuze ,waende kwa Wataalamu wa Afya kupata majibu sahihi ambayo ni ya kitaalamu zaidi.
Ndugu Mohamed Amdani almaarufu kwa Jina la Shakira, mwenye umri wa miaka 74, ni miongoni mwa wakazi wa Halimashauri ya Manispa ya Tabora waliopata fursa ya kupata chanjo hii na amewasihi wazee wenzake waje kuchanja, kwani chanjo ni kinga na anawasihi wasiogope.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt. Yahaya Nyawanda aliwaongoza wakazi wa Manispaa ya Tabora kupata chanjo hii ya UVIKO-19 huku akiambatana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri akiwemo Katibu Tawala, Kaimu Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, zoezi lililofanyika katika Kituo cha Afya Maili Tano,kata ya Ipili.
Mwisho.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.