Shirika lisilo la Kiserikali la Nchini Uingereza (HAKIELIMU) lenye Makao Makuu yake Jijini Dar es Salaam limekabidhi miundombinu ya majengo ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Mil. 140 ikiwa ni matundu ya vyoo, vyumba maalumu vya wasichana kwa ajili ya kubadilishia pedi pamoja na bweni moja la wasichana.
Akitoa shukurani kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian alisema analishukuru sana shirika la HAKIELIMU kwa kuweza kuchangia maendeleo ya Manispaa ya Tabora kwa kujenga miundombinu ya majengo ambayo yatachangia kwa kiwango kikubwa ukuwaji wa elimu kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu hasa kwa watoto wa kike.
Mhe. Dkt. Batilda aliwaeleza HAKIELIMU kuwa watoto wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwamo mazingira ya umbali kutoka majumbani kwenda shule, hivyo uwepo wa bweni hilo la wasichana kutasaidia sana kuwaondolea changamoto walizokuwa wakikutana nazo njiani, na pale wanapokuwa kwenye hedhi jambo lilikuwa linawalazimu kutohudhuria masomo.
“Kipekee kabisa niwashukuru sana HAKIELIMU kwa kuwezesha miundombinu hii ya Elimu ili watoto wetu waweze kupata huduma hizi bora wakati huo wakiendelea na masomo yao bila kurudi nyumbani kwa ajili ya kubadilisha pedi,” alisema Mhe. Dkt. Batilda.
Mhe. Dkt. Batilda alitumia fulsa hiyo kuwaonya wanafunzi wote kujiepusha na uhusiano wa kimapenzi wakiwa shuleni, na pia kujiepusha kabisa na uhusiano wa jinsi moja jambo ambalo ni hatari sana kwa wanafunzi na kuwataka waalimu kulikemea kwa nguvu zote kwenye shule zao.
Aidha Mhe. Batilda aliwahakikishia HAKIELIMU kuwa miundombinu hiyo waliyopewa watailinda kwa nguvu zote ili ije kuwa na tija zaidi hata baadae ambapo na vizazi vijavyo vinufaike, kwakuwa elimu haina mwisho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa HAKIELIMU Dkt. John Kalage aliwapongeza sana Manispaa ya Tabora kwa kuweza kupata miradi sita kutoka shirika lao la HAKIELIMU, na kwamba wameitendea haki kwakuwa kukamilika kwa miradi hiyo kunaenda kupunguza kabisa kama siyo kuondoa kabisa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi. Aidha Dkt. Kalage alimuahidi mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuwa shirika la HAKIELIMU litaendelea kushirikiana na uongozi wa Mkoa ili kwenye miradi ijayo pia waweze kuileta tena Tabora.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda aliwashukuru na kuwapongeza pia HAKIELIMU kwa msaada huo wenye thamani ya zaidi Mil. 140 na kwamba miradi hiyo inaenda kuongeza tija kubwa kwa wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu kwa ujumla.
“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Tabora, tunawashukuru sana HAKIELIMU, tunawapongeza sana na mwisho tuna waahidi kuwa tutailinda miundombinu hii na kuitunza ili isaidie na watoto wetu wa baadae,” alisema Dkt. Nawanda.
Mhe. Dkt. Nawanda alitumia fulsa hiyo pia kuwaomba wazazi wa wanafunzi wa Itonjanda kufikia tarehe 31/3/2022 kuwa wameleta wanafunzi wao na kujaza nafasi zilizo wazi kwenye bweni, na baada ya hapo kama watashindwa basi atatoa nafasi hizo wazi kutoka kwenye shule nyingine.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.