Naibu Waziri Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul ameipongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi kwa wanafunzi wote wakiwepo wenye mahitaji maalum.
Naibu waziri Gekuli amesema utekelezaji huo umeleta tija katika kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalam kitaaluma na kimichezo kuanzia ngazi ya shule hadi Kitaifa.
Pongezi hizo amezitoa Agosti 8, 2022 Mjini Tabora katika ufungaji wa mashindano ya michezo kwa Shule za Msingi (UMITASHUMNTA) yaliyofanyika kitaifa Mkoani humo.
“Niwapongeze sana Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa kuhakikisha uwepo wa fursa sawa na mazingira rafiki kwa wanafunzi wote shuleni umezingatiwa ,hii imetuhakikishia kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanashirikishwa kimichezo kuanzia ngazi ya shule hadi taifa” amesema Gekul
Pamoja na pongezi hizo Gekul ametoa rai kwa wazazi na wamiliki wa shule binafsi kuruhusu wanafunzi kushiriki katika mashindano ya michezo ili kujiimarisha kimichezo na kiafya.
Naye Naibu Katibu Mkuu Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amewataka walimu pamoja na viongozi wa michezo kujiwekea mikakati ya kuhakikisha vipaji vilivyooonekana katika mashindano ya UMITASHUMNTA 2022 vinaendelezwa na taarifa za wanafunzi hao kimchezo ziwe zinafuatiliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Batilda Buriani ameishukuru Serikali kuleta mashindano hayo katika Mkoa wa Tabora , kwani yamewanufaisha wananchi wa Tabora kiuchumi na kuahidi kujipanga zaidi kwa mwaka 2023.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.