Na Alex Siriyako:
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt.Batilda Buriani amewaasa kina mama na vijana wa kike kuchukua fomu za kugombea nafasi yeyote ya uongozi katika chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2024 na 2025.Katika kuwahimiza kwenye hilo,amewakumbusha kuwa toka harakati za uhuru wanawake kama Bibi Titi Mohamed walikuwa mstari wa mbele, hivyo historia inaonesha kuwa wanawake ni viongozi toka kwenye harakati za uhuru.
Dkt.Batilda ametoa nasaha hizi leo Machi 8, 2024 katika viwanja vya majimaji, Wilayani Igunga, Mkoani Tabora wakati akihutubia Wananchi waliofurika viwanja hivyo kuadhimisha siku ya Mwanamke Duniani, maadhimisho ambayo kimkoa yamefanyika wilaya ya Igunga.
Amefafanua kuwa, Tanzania ni miongoni mwa Nchi chache Duniani ambazo zimepiga hatua kubwa ya usawa wa kijinsia, na kuongeza kuwa Tanzania ina Rais Mwanamke, Mawaziri, Viongozi mbalimbali kila sekta, hatua ambayo kuna Nchi nyingi zenye uchumi mkubwa na bado hazijafika hapa Tanzania ilipo.
Aidha Dkt.Batilda ametanabaisha kuwa uchumi wa mwanamke unastawi mahala penye amani, hivyo kama Watanzania hatuna budi kuilinda tunu ya amani tuliyonayo ili tuweze kufanya kazi zetu za kiuchumi vizuri. Ameongeza kuwa Rais Samia anapambana kuimarisha uchumi kwa ngazi zote kwa vitendo, na kwa kinamama na vijana wa Tabora Rais ameahidi kuleta kiwanda cha kutengeneza mizinga ya nyuki ili kupunguza gharama ya sasa ya utengenezaji wa mizinga hiyo kutoka Tsh.120,000/= hadi Tsh.40,000/= kwa mzinga mmoja.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa Rais Samia katika kuunga mkono uwekezaji kwa mwanamke na Jmii kwa ujumla, ametoa zaidi ya milioni mia mbili kwaajili ya mafunzo kwa vijana 23 wa Mkoa wa Tabora ili wapate ujuzi wa kuchakata mazao ya pamba na hatimae waweze kutengeneza bidhaa mbalimbali kama nguo na bidhaa zinginezo.
Historia ya Siku ya Mwanamke Duniani ilianzia mjini New York-Marekani, ambapo wanawake takribani 15,000 waliandamana kudai haki ya ujira mzuri, wapunguziwe muda wa kufanya kazi pamoja na haki ya kupiga kura. Mwaka 1910 Mwanamama Clara Zetkin akatoa wazo la kuadhimisha siku hii kuwa ya Kimataifa, na hatimae mwaka 1911 kwa mara ya kwanza, siku hii ya Mwanamke iliadhimishwa Kimataifa kwa mara ya kwanza.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.