Na Paul Kasembo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amezindua rasmi Baraza la Biashara ya Wilaya ya Tabora lenye lengo la kujenga uelewa na mtazamo wa pamoja kuhusu masuala muhimuya maendeleo kati ya Sekta hizi mbili.
Akizindua Baraza hilo Balozi Dkt. Batilda aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo pamoja na wadau mbalimbali waliohudhurio kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuwa, uwepo wa Baraza hilo utawezesha utekelezaji wa Mwongozo utapelekea uwepo wa mazingira wezeshi kibiashara, kutajenga na kuaminiana miongoni mwa wadau na hivyo kuifanya Sekta Binafsi kuwa endelevu zaidi.
“Sisi Serikali tunawahakikishieni mazingira rafiki, wezeshi na salama kwenu nyinyi wadau wa Sekta Binafsi kwenye shughuri zenu kwani kufanikiwa kwenu ndiyo kufanikiwa kwa Serikali pia”, alisema Dkt Batilda.
Balozi Dkt. Batilda alisisitiza kuwa mabaraza ya biashara yameanzishwa kwa mujibu wa sheria mnamo mwaka 2001, na Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, amezindua rasmi Balaza la Biashara Kitaifa, na akaagiza mabaraza ya biashara kwa ngazi za Wilaya yaundwe na yaanze kazi mara moja.
Aidha aliwataka wadau wote kuzibaini na kuzitumia vema fulsa zilizopo kwenye Wilaya ya Tabora zikiwamo kilimo cha Alizeti, Pamba, Tumbaku, Karanga, Mahindi na kwa sasa kuna kilimo cha Mikorosho ambacho kinakubali katika maeneo mengi hapa Wilaya ya Tabora pia kuanziasha kilimo cha Michikichi ili kukidhi mahitaji ya mafuta ya kula.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dkt Yahaya Nawanda alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa jambo hilo na kisha kuelekeza pia litekelezwe katika Wilaya ambapo kwa Wilaya ya Tabora uzinduzi ndiyo unafanyika, kisha akamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kukubali kuja kuwa Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi huo na mwisho aliwashukuru sana wadau wote wa Sekta Binafsi kwa muitikio wao kuja kwenye uzinduzi.
Kando na uzinduzi pia Dkt. Batilda alitmia fulsa hiyo kuwaeleza wadau na wajumbe hao juu uwepo wa maandalizi ya uzinduzi wa loti ya tatu na ile ya nne ya ujenzi wa Reli ya mwendo kasi, kwenye loti ya tatu itaanzia Makutupora-Singida mpaka Tabora, na Loti ya nne itaanzia Tabora mpaka Isaka-Shinyanga. Fulsa hiyo itakwenda sambamba na fulsa ya ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Nchi ya Uganda mpaka Tanga-Tanzania ambao utaanza siku za usoni, ambapo bomba hilo linapita Wilaya za Nzega na Igunga Mkoani Tabora, amefafanua zaidi kwamba kambi kubwa itakuwepo Nzega hivyo itatoa fursa za ajira kwa wakazi wa Tabora pamoja na fulsa za biashara za vyakula mbalimbali.
Dkt.Batilda alihitimisha hotuba yake fupi kwa kuwataka Uongozi wa Wilaya ya Tabora kumpelekea ratiba ya vikao vya Baraza hili la biashara kwa mwaka mzima,ambapo baraza linakaa mara nne kwa mwaka, vilevile kama wilaya wakae waandae mpango wa utekelezaji wa mpango mkakati wa Mkoa, na mwisho kabisa akatoa rai kwamba suala la Sekta Binafsi liwe chachu ya maendeleo na litafsiriwe kwa vitendo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.