Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Komanya Kitwala leo tarehe 19.1.2021 amezindua shughuli za uhamasishaji wa Bima ya Afya ya Jamii yaani CHF iliyoboreshwa kwa wananchi wa Tabora Manispaa.
DC Komanya amezindua shughuli hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo Shule ya Sekondari ya Mihayo ambapo alikuwa ameambana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Viongozi wa Vyama na wataalamu mbali mbali kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Akihutubia Mkutano huo mkubwa ambao pia ulikuwa umejumuisha Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji, Vitongoji na Viongozi mbalimbali wa taasisi za kidini, Komanya aliwaeleza kuwa Tabora Manispaa bado hajakuwepo na muitikio mzuri kwa wananchi kujiandikisha kwenye huduma ya Bima ya Afya ya Jamii kwa sababu katika Tabora Manispaa hapakuwa na utoaji wa elimu ya kutosha juu upatikanaji wa Bima ya Afya ya Jamii yaani CHF ILIYOBORESHWA jambo ambalo limenisukuma kuwaiteni hapa ili tupeane elimu na tuende tukahamasishe wananchi wetu, waumini wetu na wakazi wetu kila mmoja kwenye eneo lake ili tuweze kuwasaidia kupata huduma hiyo na kuokoa maisha yao.
Aidha Komanya alisema kuwa, viongozi wote wa kidini, kisiasa, na wa kiserikali wanao wajibu wa kuelimisha na kuhamasisha bila kuchoka kwakuwa hiyo jamii wanayoishi nayo ina hatma kubwa ya ukuaji wa kiuchumi, kijamii na kiustawi kwakuwa kama itakuwa haina uhakika wa afya basi hayo yote yatakuwa hayana maana yoyote kwakuwa hayataweza kutekelezeka.
Kando na hayo, pia DC Komanya alitumia fulsa hiyo kuwaagiza Watendaji wote wa Kata, Mitaa na Vijiji kwenda kuifanya ajenda ya Bima ya Afya kuwa ni ya kudumu kwenye vikao na mikutano yao yote kuanzia sasa ambapo watapaswa kutoa elimu na hamasa kwa wajumbe na wananchi wao.
Awali akisoma taarifa ya UTEKELEZAJI WA HUDUMA ZA CHF ILIYOBORESHWA ndugu Nehemia Steven ambaye ni Mratibu wa CHF ILIYOBORESHWA kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora alimueleza Mhe. Komanya kuwa Manispaa ina lengo la kuandikisha wanachama kwenye kaya 47,922 zenye wastani wa wanufaika 287,532 ambapo tangu wameanza kuandikisha ni kaya 921 zimekwisha andikishwa zenye wanufaika 5,339 ambayo ni sawa na asilimia 2 ya lengo kuu na kwamba kwa mwaka huu wa 2021 Halmashauri imejiwekea lengo la asilimia 10 ya uandikishaji wananchama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Mohamed Katete alimpongeza sana Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa namna ambavyo amekuwa mbunifu na mfuatiliaji wa kazi zake za kila siku tangu afike Tabora Manispaa na kwamba amewezesha mambo mengi kwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Halmashauri, kuboresha miundombinu ya Elimu na Afya na kwamba hana shaka na hili la Bima ya Afya litakwenda vizuri sana.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.