Mstahiki Meya wa Tabora Manispaa Mhe. Ramadhani Kapela leo amekutana na baadhi ya wafanyabiashara wa vileo Tabora Manispaa na kufanya nao mkutano ambapo waliweza kujadiliana mambo mbali mbali ikiwamo changamoto na fulsa wanazokutana nazo kwenye biashara yao.
Katika kikao hicho ambacho kilifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Manispaa kilianza kwa kupata utambulisho kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ndg Seif Salumu, wataalamu wa Manispaa pamoja na wafanyabiashara kuliweza kuibuliwa hoja kadhaa ambazo Mstahiki Meya alimtaka Kaimu Mkurugenzi na wataalamu wake kuzitoela ufafanuzi ili kuweza kuondoa shaka walizonazo wafanyabiashara hao.
Sehemu kubwa ya hoja walizoelezea wafanyabiashara ilikuwa ni muda wa kufungua na kufunga biashara zao hizo kuwa ni mfinyu sana kulinganisha na biashara nyingine, ambapo Kaimu Afisa Biashara aliweza kuwakumbusha sharia, kanuni na miongozo inayo ongoza biashara ya vileo.
Kwamba kwa sehemu kubwa biashara hiyo hupaswa kufunguliwa kuanzia saa kumi za jioni na kufungwa saa sita kamiili za usiku hiyo ni kwa siku za kawaida, ambapo kwa siku za mapumziko na sikukuu mfanya biashara huruhusiwa kufungua kuanzia saa sita mchana na kufunga ifikapo saa sita usiku.
‘’ sharia ya biashara ya vileo ipo wazi sana na tena imeandikwa kwa Kiswahili ambapo mfanyabiashara hupaswa kuifuata ili aweze kuendesha biashara yake bila usumbufu, lakini pia anaweza kuzidisha muda uliotajwa kwenye iwapo tuu mfanyabiashara huyo atakuwa ameomba kibali ambacho kulingana na mazingira ya tukio lenyewe kumlazimu kuzidisha muda laakini vinginevyo sharia ndivyo inataka kufuatwa,’’ alisema Festo Kaimu Afisa Biashara.
Aidha katika hatua nyingine wafanyabiashara hao waliishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeweza kufungua njia za kuingia na kutoka Tabora Manispaa na hivyo kuifanya biashara yao kupata wateja wengi Zaidi tofauti na awali ilivyokuwa, kwakuwa hivi sasa kuna basi za Mikoani huingia na kutoka mpaka usiku ukijumlisha na Treni ya abiria ambayo pia huteremsha abiria wengi na hivyo kupelekea muongezeko wa wateja wa vinywaji.
Kwa upande wake Mstahiki Meya aliwaomba wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano mkubwa kwa wataalamu wa Manispaa ambao huwafikia mara kwa mara kwenye maeneo ya biashara ili kuweza wakifanya hivyo kutawezesha kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto wanazokutatana nazo na hivyo kutapelekea wao kuweza kulipa kodi Serikalini kwa wakati na kuongeza mapato ya Halmashauri kwa ujumla.
Huu ni mwanzo wa juhudi za Mstahiki Meya katika kutekeleza ahadi zake za kuitoa Manispaa hapa ilipo na kuisogeza mbele Zaidi kimaendeleo kwa kukutana na makundi ya wafanyabiashara mbalimbali Tabora Manispaa akiwa na lengo la kuwataka kushirikiana na Serikali ya Manispaa kwa kila upande kutekeleza wajibu wake ambao mwisho utakuwa na tija hasa kwa kuongeza mapato kwenye Manispaa na hivyo kuboresha huduma kwa jamii yote ya Tabora Manispaa.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.