Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Komanya Kitwala amewaambia Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kuwa wanao wajibu mkubwa wa kuwa karibu na kuwatumikia wananchi wao wote waliowachagua na ambao hawakuwachagua tena bila ubaguzi ili waweze kuwaletea maendeleo.
Hayo yamesemwa leo kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano uliopo Shule ya Sekondari ya Mihayo na kuliohudhuriwa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji wote waliochaguliwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Kwenye Mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala aliwaekeza Wenyeviti hao kuwa wanatakiwa kwenda kuishi na kutekeleza yafuatayo; kwenda kusaidia kutatua migogoro hasa inayohusu Ardhi. Kumekuwa na migogoro mingi sana hasa inayohusu Ardhi ambapo unakuta migogoro hiyo inachangiwa na Wenyeviti wenyewe na wengine hawashughuriki ipasavyo kuitatua kwa maslahi mapana ya wananchi.
‘’Saidieni kutatua migogoro hasa ya Ardhi kwenye maeneo yenu. Haiwezekani Viongozi wote wapo hapo, yaani kuna Mtendaji wa Mtaa, Mwenyekiti yupo lakini bado kuna migogoro ya Ardhi mpaka inafikia wakati wanalazimika kuja Ofisi ya Mkuu wa Wilaya au kwenye Ofisi ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Tabora Mjini’’, alisema Komanya.
Matumizi mabaya ya madaraka: Mkuu huyo wa Wilaya aliendelea kuwaelekeza Wenyeviti hao kwenda kutumia vizuri madaraka waliyonayo na siyo vinginevyo. Viongozi wote mliochaguliwa mkienda kutumia madaraka vibaya mtachomolewa haraka sana, badala ya kwenda kutatua matatizo na kusaidia wananchi, wao wanaenda kuwanyonya wananchi na kutumia madaraka yao vibaya.
‘’Nafasi ya Mwenyekiti ni nafasi ya kuwatumikia wananchi na siyo sehemu ya kwenda kujilipa mamilioni ya pesa na kupora Ardhi za watu, muhuri wako, nafasi yako ukienda kuitumikia vibayatutaunda timu ikuchunguze na ukibainika tutakutoa na kuitisha uchaguzi mwingine, maana haufai’’, Komanya.
Kuchelewesha kutoa maamuzi yenye maslahi kwa umma na kusimamia uwajibikaji: Viongozi mnatakiwa kufanya maauzi yenye nia njema kwa umma, unakuta ukweli upo wazi na unaonekana kabisa lakini kunakuwa na ucheleweshwaji mkubwa wa kutoa maamuzi kwa wakati.
Ambapo alitaja baadhi ya maeneo yenye kuchelewesha utoaji wa maamuzi kama vile kata ya Mwinyi, Malolo,Mtendeni, Uyui na maeneo mengine. Hivyo aliwaasa sana Wenyeviti hao kwamba kuna kila sababu ya kutoa maamuzi kwa wakati, khivyo wakafanye maamuzi kwa maslahi mapana ya wananchi wao na wasiogope kutishiwa kwakuwa wanatenda haki.
Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo: Kwenye hili aliwataka Wenyeviti wote kwenda kusimamia Miradi yote iliyopo kwenye maeneo yao kwa ajili ya maslahi makubwa ya Taifa letu ili mwisho wa siku kuwepo na mifano bora ya usimamizi huo. Komanya alitoa mifano ya sehemu zilizofanya vizuri ni kama vile Shule ya Msingi Kanyenye, Kwihara, Isike, Mpepo mnaweza kuona ni jinsi gani usimamizi unapokuwa mzuri na matokeo yake yanakuwa ni mazuri sana. ‘’Nendeni mkasimame kwenye nafasi zenu vizuri ili Manispaa yetu isonge mbele kwakuwa tunao mpango wa kujenga madarasa na tutaleta matofali, nendeni mkawasimamie ujenzi huo na muwahamasishe wananchi wenu yote inawezekana tukiamua’’, alisema Komanya.
Kwa upande Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru alisema kwanza kule kuna kazi za Watendaji na zile za Wenyeviti hivyo mkashirikiane wote kutekeleza yote yaliyoelekezwa na viongozi wetu. Pili, mambo yote yanafuata kanuni, taratibu na sheria hivyo pale unapokwama na hauna uhakika ni vema ukaulizia sheria inasemaje ili usije kuonekana unayoyafanya yaonekane yapo kwa mujibu wa sheria na uzuri ni kwamba mawasiliano yapo.
La mwisho, kila unapofanya shughuri za utekelezaji kunahitaji mawasiliano, kitu gani kinachohitajika na bahati nzuri kuna ngazi mbali mbali hapo.
’’Sasa basi Wenyeviti kama ni wa Mtaa lazima umtaarifu Mtendaji wa Kata ili ifike huku, siyo kila kitu unakipiga huku juu na kama itakuwa hivyo basi mpe nakala wa eneo husika ili nay eye afahamu, mfano kuna mgogoro basi mpe nakala ili isionekane ni majungu tuu’’, alisema Ndunguru.
Mkutano huo wa Mkuu wa Wilaya na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji ulihudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wakiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tabora Mjini Mohamed Katete, Katibu wa CCM Tabora Mjini Adam Makulilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Tabora Mjini Rashid Ramadhani (Tall), Katibu Tawala Tabora Mjini H. Yonaza, Afisa Uchaguzi Msaidizi Tabora Manispaa pamoja na Waandishi wa habari mbali mbali.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.