Mkuu wa Wilaya Tabora Mjini Mhe Komanya Kitwala amekabidhi Vitambulisho 12,000 vya Wajasiliamali kwa Watendaji wa Kata 29 Tabora Manispaa ambavyo vitauzwa kwa Wajasilimali wadogo wadogo watakaokuwa na vigezo kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
DC Komanya amekabidhi Vitambulisho hivyo kwenye hafla fupi ambayo ilifanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Tabora ambapo palihudhuriwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndg. Bosco Ndunguru, Wakuu wa Idara, Vitengo, Afisa Tarafa Kusini pamoja na Watendaji wa Kata.
Akikabidhi vitambulisho hivyo DC Komanya alitaka Watendaji Kata wote kwenda kuifanya kazi hiyo kwa uadilifu, umakini na uaminifu mkubwa kwakuwa itahusisha ukusanyaji wa pesa kutoka kwa Wajasiliamali hao na kuzipeleka Serikalini.
‘’Nendeni mkaifanye kazi hii kwa uadilifu mkubwa, uaminifu na umakini mkubwa kwakuwa mnaenda kushika pesa za Serikali na maisha ya watu ambao ndiyo hao wajasiliamali wadogo wadogo, na mhakikishe kuwa wanaopewa ni wale wenye vigezo peke yake kwa mujibu wa maelekezo ya Serkali na siyo vinginevyo na mkaifanye kazi kwa mfumo wa ushirikiano kama timu moja,’’ alisisitiza DC Komanya.
Akipokea vitambulisho hivyo kwa niaba ya Halmashauri, Mkurugenzi wa Manispaa Ndg. Bosco Ndunguru alimshukuru Mhe Komanya kwa maelekezo hayo na akamhakikishia kuwa kazi hiyo itaenda kutekelezwa kwa uangalifu na usimamizi mkubwa sana na kwamba yeye mwenyewe kama Mkurugenzi atafuatilia kwa ukaribu zaidi zoezi hilo.
Vitambulisho hivyo vilivyopokelewa ni sehemu ya muendelezo wa zoezi la Serikali kuwasaidia Wajasiliamali wadogo wadogo Nchini ambapo kwa mara ya kwanza vilianza kutolewa mwaka 2019 Januari kwa lengo la kuwaondolea usumbufu na kero wakati wa kufanya biashara zao na pia Serikali kuwatambua Wajasiliamali wadogo wadogo kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.