Na Alex Siriyako:
Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Deusdedith Katwale ameepa kutokomeza foleni za Wanamchi wanaotaka huduma katika taasisi mbalimbali za umma, Vituo vya kutolea huduma za afya hasa vya umma pamoja na Ofisi mbalimbali za Serikali.
Mhe.Katwale amefafanua kuwa, Wananchi ndio wameiweka Serikali madarakani, hivyo haipendezi na sio sawa kuwaona wanapoteza muda wao mwingi kwenye foleni wakisubiri huduma huku na wengine wakiwa ni wagongwa kwenye vituo vyetu vya huduma za afya.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa Kiongozi, Afisa wa Serikali na mtoa huduma yeyote yule kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma stahiki na kwa wakati na kumpa muda wa kwenda kufanya kazi zingine za kujenga Taifa.
Mhe.Katwale ametoa rai hii leo Machi 13,2024 katika ukumbu wa Manispaa ya Tabora katika kikao chake cha kwanza kabisa na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Wilaya ya Tabora baada ya kuwasili katika Wilaya aliyohamishiwa (Tabora) akitokea Wilaya ya Chato alikokuwa akifanyia kazi kwa nafasi kama hii ya Mkuu wa Wilaya.
Aidha Mhe.Katwale ametanabaisha kuwa, angetamani sana Manispaa ya Tabora kuwa Jiji, kwani Manispaa ya Tabora ni miongoni mwa Manispaa za kwanza kabisa Nchi hii, lakini bado inaendelea kuitwa Manispaa hadi leo, hali ambayo haileti tija kwa wakazi wa mji huu.
Katika kuonesha nia yake thabiti ya kupambana kuitoa Manispaa ya Tabora hatua moja kwenda hatua nyingine, Mhe.Katwale amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora (ambaye amewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi, Mhifadhi Sefu Salumu) ndani ya wiki moja kuwasilisha mezani kwake mpango mkakati wa kuitoa Manispaa ya Tabora hapa ilipo na kuwa Jiji.
Mhe.Katwale amesisitiza kuwa hana itifaki kwenye ufuatiliaji wa maslahi ya Wananchi na atatoa ushirikiano kwa kila Mtanzania bila kujali cheo chake na nafasi yake, Zaidi amefafanua kuwa kikao cha leo ni kwaajili ya kufahamiana, ili kazi na majukumu mengine yaweze kuendelee vizuri.
Amehitimisha kikao hiki kwa kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini katika nafasi hii kwa awamu nyingine tena, na amewashukuru Wanatabora kwa mapokezi mazuri na kusisitiza tena atatoa ushirikiano wa kutosha kuwatumikia Wananchi.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.