VIONGOZI wa Serikali za mitaa waliochaguliwa wametakiwa kuwahudumia wananchi bila ya upendeleo wowote na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ndiyo chanzo cha migogoro kwenye maeneo yao ya utawala.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala Wilaya ya Tabora Mjini Hammarskjold Yonaza wakati wa zoezi la kuwaapisha viongozi hao wa mita lilifanyika kwenye ofisi za Manispaa hiyo.
Yonaza aliwaeleza viongozi hao wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa kuwa wakitoa haki bila upendeleo itasaidia sana kutimiza ndoto za wananchi wanaowaongoza na waliowachagua ili waweze kuwaletea maendeleo yao na pia kuishi bila migogoro.
“Hakika msipotenda haki ina maana mtakuwa mmeshindwa kuongoza na kutoa fursa ya kuwepo migogoro kwenye maeneo yenu jambo ambalo halikubaliki kabisa hasa kwenye Serikali hii ya awamu ya tano,” alisema Yonaza.
Aidha Katibu Tawala aliwaonya wachaguliwa kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo kwa namna moja au nyingine vyaweza kuwa vinasababisha kuzalisha migogoro katika jamii na kuwatia aibu wao wenyewe pindi watakapobainika.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manisapaa ya Tabora William Mpangala alisema kuwa Manispaa ina jumla ya Mitaa 134, wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) 126 walipita bila kupingwa na Mitaa 8 ndio iliyofanya uchaguzi ambapo wagombea wa Chama hicho walishinda.
Aidha Mpangala alisema kuwa Chama cha Mapinduzi pia kilinyakuwa viti vyote vya wenyeviti wa vijiji 41 na vitongoji 156 baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa.
Viongozi hao wameapishwa leo tarehe 26/11/2019 na Hakimu wa Wilaya ya Tabora Seraphina Nsana kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi za Manispaa ya Tabora.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.