Na Alex Siriyako:
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora Bi. Asha Churu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Deusdedith Katwale amewataka wadau mbali mbali wa maendeleo kama Taasisi Binafsi, Mashirika ya Umma pamoja na Watu Binafasi kujitoa kwa kuwapatia wanafunzi hasa walio na umri wa miaka miatano vyakula vyenye virutubisho kama maziwa, lengo likiwa ni kupambana na udumavu na utapiamlo kwa watoto, hasa wale wa makundi maalumu.
Bi. Churu ametoa wito huu leo Septemba 18, 2024 katika shule ya msingi Furaha, ambayo pia ni shule ya watoto wenye mahitaji maalumu, ambapo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, amezindua program ya kuwapa watoto wa shule hasa za msingi na awali maziwa katika Manispaa ya Tabora ili kupambana na hali ya udumavu na utapiamlo kwa watoto hasa wanaosoma.
Programu hii imezinduliwa leo kwa kuwapatia maziwa yaliyosindikwa watoto wa shule za Furaha, Kizigo na Ipuli, lakini pia program hii kwa awamu hii ya kwanza inalenga kuzifikia shule za msingi na awali kumi na moja (11) zilizopo Manispaa ya Tabora, ambapo chupa 870 zimelengwa kugawiwa kwa watoto katika shule hizo, huku watoto wanaolengwa zaidi wakiwa ni wale waliochini ya miaka mitano pamoja na wale wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndugu Elias Kayandabila ameeleza kuwa, mpango wa kuwapatia watoto wa shule maziwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo amezitaka Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya masuala ya lishe.
Ndugu Kayandabila amefafanua kuwa ziko AFUA ZA LISHE mbalimbali ambazo Halmashauri inatekeleza, hivyo ugawaji wa maziwa ni sehemu tu ya AFUA hizo, ambapo zote kwa pamoja zinalenga kutokomeza kabisa suala la udumavu na utapiamlo kwa watoto hasa walio chini ya miaka mitano, lakini pia na wananchi ambao ni wakubwa wanapaswa kupata milo yenye virutubishi vyote vya msingi katika milo yao ya kila siku.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.