Baraza maalumu la waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya manispaa ya Tabora leo tarehe 16 Juni, 2021, limepata wasaa wa kuijadili na kupata ufafanuzi wa kutosha kuhusu repoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Baraza hilo kiitifaki limehudhuliwa na viongozi mbalimbali kwa nafasi zao ;wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa Tabora Ndg Msalika Makungu, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa Ndg Hamu Mwakasola, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Mhe. Komanya Erick Kitwala, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Katibu Tawala wa Manispaa Tabora Ndg Hammasrsjold Yonaza, waheshimiwa madiwani, wawakilishi wa vyama vya CCM na CHADEMA, wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali, watendaji wa Kata zote pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbal.
Repoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ilikuwa na jumla ya hoja 158, ambapo kati ya hoja hizo, hoja 83 ni za miaka ya nyuma na baada ya uhakiki hoja 73 zimepatiwa majibu ya kuridhisha na kufungwa na kusalia na hoja 85 ambazo ni sawa na asilimia 54.
Mkaguzi wa hesabu za serikali Mkoa alieleza kwamba, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Tabora ilipata hati chafu yaani Adverse Opinion. Na hii ilitokana kwa asilimia kubwa kwa kutokufuata miongozo ya kimataifa ya uandaaji wa hesabu za taasisi za umma yaani IPSAS ambazo kama Nchi tumeridhia kuzifuata.
Vilevile, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa aliendelea kueleza kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali sio wa kuridhisha sana na hivyo akaitaka menejiment ya Manispaa ya Tabora ifanye jitihada za dhati kufanyia kazi mapendekezo hayo. Namnukuu.
“Nitoe lai kwa menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali alisisitiza Mwakasola.”
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Ndugu Msalika Makungu alielezea kuwa sehemu kubwa ya chanzo cha kupata hati chafu ni uzembe mkubwa unaofanywa na baadhi ya watumishi wa Manispaa hasa wakuu wa idara, jambo ambalo haliwezi kuendelea kuvumiliwa.
“Hivi jamani hata suala la kupeleka asilimia kumi kwenye vikundi pamoja na kutenga asilimia arobaini kwa ajili ya maendeleo, au kununua bidhaa na kuweka stoo bila kuingiza kwenye reja pamoja na nyingine nyingi, hizi ni miongoni mwa hoja za kizembe zilizosababisha Halmashauri kupata hati chafu pasipo na sababu za msingi.”
Hivyo akaitaka Menejimenti kubadilika na kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita, na kwamba tabia za kizembe kama hizo zinazopelekea Halmashauri kupata hati chafu au yenye mashaka zisijirudie tena.
Aidha kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa Tabora, Mheshimiwa Ramadhani Kapela akihitimisha Baraza kwa kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa na Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kuweza kufanikisha kufunga hoja zote zilizosalia hususani za mwaka wa fedha 2019/2020. Aliwaasa wakuu wa Idara mbalimbali na watumishi wote wa Manispaa ya Tabora kuwa kitu kimoja na kufanya juhudi kubwa za kuipandisha hadhi zaidi Manispaa na iweze kufikia malengo ya kutoa huduma kwa wananchi wake.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.