Baraza maalumu la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limeazimia kuwapa wiki mbili Menejimenti ya Halmashauri kuhahakisha inaanza kuwakata kwenye mishahara watumishi wanaodaiwa masurufu yenye thamani ya shilingi milioni 4.7 pesa ambazo zimepelekea kuzalishwa kwa hoja ya Mkaguzi na Mdhiti Mkuu wa Serikali CAG kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Agizo hilo limetolewaleo na Baraza la Madiwani Manispaa ya Tabora baada ya kupokea pendekezo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani ya kupitia hoja ya mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2017/18.
Madiwani walikubaliana kwa kauli moja kwamba ndani ya wiki watumishi wote wanaodaiwa wahakikishe wamelipa fedha hizo au wakatwe kwenye mishahara yao.
Walisisitiza kwamba iwapo wasipokatwa fedha hizo hoja hiyo itaendelea kujitokeza na hivyo itapelekea muendelezo wa kuchafua hesabu za Manispaa ya Tabora na heshima yake pia.
Pamoja na hilo Baraza la Madiwani pia lilikubaliana na agizo la Mkuu wa Mkoa huyo ambalo linawataka Wakuu wa Idara kuhakikisha wamefanyia kazi hoja zote za CAG ndani ya wiki mbili tuu na kuwalisilisha vielelezo vyote ili hoja ziweze kufungwa .
Mkuu wa Idara ambaye ndani ya kipindi hicho atashindwa kujibu hoja hizo na kusababisha kuendelea kuwepo atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa katika nafasi yake, alisema Mwanri.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora amewataka uongozi wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanakusanya madeni yote ya ardhi na mikopo ya wanawake, vijana na walemavu yanayo kadiriwa kufikia zaidi ya milioni 536.
Kumekuwepo na uuzaji wa viwanja vya Halmashauri ambapo wananchi waliotakiwa kufidiwa maeneo yao hawakulipwa mpaka sasa na wale ambao walipewa viwanja wamekuwa wakilipa kidogo kidogo na hivyo kusababisha deni kuwa kubwa la kufikia zaidi ya milioni 503, na hivyo akawataka kushughurikia hilo nalo liondolewe kwenye vitabu vya CAG, alisema Mwanri.
Pia Mwanri alitumia fulsa hiyo kusisitiza ufuatiliwaji na urejeshwaji wa fedha za vikundi vya wanawake, vijana na walemavu ipatayo milioni 33.7 irejeshwe haraka ili na wengine waweze kukopeshwa.
Awali Mkuu waWilaya ya Tabora Komanya Kitwala alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa kuhakikisha kuwa anawachukulia hatua watumishi wote ambao wameisababishia Halmashauri kuzalisha hoja za kiukaguzi. Pia alisisitiza kuwepo na kuwajibishana, kutunza kumbukumbu na mwisho kuwepo na uthubutu kwa Mkurugenzi.
Watumishi wanapaswa kujitahidi kuzuia hoja zisitokee na siyo kupelekea maamuzi ambayo yanasababisha kuendelea kwa uzalishwaji wa hoja kila mwaka alisema Komanya.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.