Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora robo ya nne limeipongeza Menejimenti na Mkurugenzi wa Manispaa kwa kutekeleza vema wajibu na majukumu yao na hata kuiwezesha Manispaa ya Tabora kupata Hati Safi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akitoa pongezi hizo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Shabani Kapela aliwaeleza wajumbe wa baraza kuwa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora pamoja na Menejimenti yake wamefanya kazi nzuri sana ya kujituma kukusanya mapato hata sasa tumeweza kupata asilimia 94 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 tofauti na kipindi cha miaka ya nyuma ambapo hatukuwa tukifikia asilimia hizo.
“Kipekee kabisa baraza la madiwani likiongozwa na mimi mwenyewe Mstahiki Meya, tunatoa pongeza za dhati kwa Mkurugenzi wetu Dkt. Peter Nyanja na Menejimenti yake kwa kuweza kukusanya mapato makubwa na hata kufikia asilimia 94, tofauti kubwa tunaiona hivi sasa inatokana na Mkurugenzi wetu akisaidiwa na Menejimenti yake mfenya kazi nzuri sana tunawapongeza,” alisema Mstahiki Meya Kapela.
Aidha Mstahiki Meya alitumia fulsa hiyo kumshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anliletea maendeleo Taifa la Tanzania na kuwaunganisha watu wake. Kisha akampongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi. Dkt. Batilda Burian kwa nama ambavyo amekuwa akiwatumikia wananchi wa Mkoa wa Tabora na Wilaya zake zote.
Pongezi za kipekee kwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Esmail Nawanda kwa utumishi wake bora ulipelekea hata Mhe. Rais akaiona na kuamua kumpandisha cheo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, hakika ni furaha kubwa sana kwa wananchi wa Manispaa ya Tabora kwakuwa kupanda kwake kumetokea katika eneo ambalo wananchi walikuwa wakimpenda sana.
Akitoa shukurani zake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda aliwashukuru sana waheshimiwa madiwani wa Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mstahiki Meya Mhe. Kapela na wananchi wa Manispaa ya Tabora kwa namna ambavyo walikuwa wakisapoti katika kazi zake za kila siku katika kuwatumikia wananchi wa Manispaa ya Tabora tangu kufika kwake.
“Niwashukuru sana Waheshimiwa Madiwani wangu mkiongozwa na Mstahiki Meya wetu kwa namna ambavyo mmekuwa msaada mkubwa kwangu katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku nikiwa hapa kama Mkuu wa Wilaya, hakika nitawakumbuka sana na wala sijutii kufanya kazi hapa,” alisema Dkt. Nawanda.
Katika hatua nyingine Dkt. Nawanda aliwaomba waheshimiwa madiwani na menejimenti kwenda kuendeleza miradi waliyokuwa wameianzisha ili ije kuwa na tija kwa wananchi wa Manispaa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Maiga Nyanja aliwashukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuikumbuka Manispaa ya Tabora na hata kuiongezea fedha katika miradi mbalimbali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kuendelea kumsapoti kwenye kazi zake za kila siku, Mkuu wa Wailaya ya Tabora kwa kukubali kufanya kazi bega kwa bega hata kuweza kufikia malengo ya Manispaa katika kukusanya mapato, Mstahiki Meya kwa ushirikiano mkubwa anaompatia wakati wote wakati wa kutekeleza majukumu yake, wahe. Madiwani na watumishi na wadau wote kwa ujumla.
“Kwangu mimi nyote ni watu muhimu san katika kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya kila siku, binafisi nafarijika sana na menejimenti yangu inaungana nanyi kwenye kila maelekezo mnayotoa na mtakayoendelea kuyatoa yatatekelezwa kama mtavyoelekeza kwa asilimia mia moja, nawashukuruni sna hata kwa kuikubali Taarifa yangu ya Utekelezaji na Uwajibikaji ya mwaka fedha 2021/2022,” alisisitiza Dkt. Nynaja.
Kando na hayo, baraza pia lilifanya uchaguzi mdogo wa kumpata Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora ambapo Mhe. Nassir I. Mnenge alifanikwa kuibua mshindi na hivyo kuwa Naibu Meya ambaye atahudumu kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 akimrithi Mhe. Kasongo Amrani ambaye alihudumu kwa vipindi viwili mfululizo.
Kukamilika kwa baraza hili la mwaka wa fedha 2021/2022, kunafungua ukurasa mpya wa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Manispaa ya Tabora ikiwa na malengo pamoja na mikakati mipya katika kukusanya mapato na kuwahudumia wananchi wake wa Manispaa ya Tabora.
MWISHO.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.