NA Alex Siriyako:
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limelaani na kukemea vikali vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto hasa wa shule za Msingi katika Manispaa.
Rai hii imetolewa na Baraza la Madiwani ambalo limefanya kikao cha kawaida cha robo ya nne mwaka wa fedha 2023/2024 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora leo Agosti 12, 2024.
Ni kufuatia tuhuma za mwalimu ajulikanae kwa jina la Doto Elias Masatu kumulawiti mwanafunzi (jina linahifadhiwa) wa kiume, mwenye umri wa miaka saba (7) anaesoma darasa la pili katika shule ya msingi Saint Doroth iliyopo Kata ya Mtendeni katika Manispaa ya Tabora.
Tukio hili limebainika siku chacha zilizopita na tayari uongozi wa Mkoa wa Tabora chini ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Matiko Chacha umeshatoa maelekezo na Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea na uchunguzi na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kumuweka mahabusu mtuhumiwa huyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoani Tabora pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa hatua ambazo wameshazichukua, lakini pia ameomba watu wanaozunguka na kwenda kwa mama mzazi wa mtoto anaedaiwa kulawitiwa na kumshawishi wayamalize nje ya mahakama nao wakamatwe na ikiwezekana washitakiwe pia.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tambukareli, Mhe. Zinduna Kisamba ambae pia ni Katibu wa Jumuia ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tabora, ameeleza jinsi ambavyo wao kama wazazi na viongozi wamesikitishwa na tukio hilo, na ametoa ushauri na maoni yake kuwa watu wenye tabia chafu kama hizi ni vyema wakahasiwa, kwani hata huko gerezani wanaendeleza michezo hii michafu, na hata wakimaliza adhabu yao wakirudi uraiani kuna uwezekano mkubwa sana wa kuendeleza tabia hizi.
Pamoja na agenda nyingi zilizojadiliwa, Baraza limepokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shuguli za maendeleo katika Kata ishirini na tisa (9) za Manispaa ya Tabora, na kwa pamoja Waheshiwa Madiwani wameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi ya kutosha katika kata zote za Manispaa ya Tabora inayoendelea kutekelezwa na iliyokamilika hivi karibuni.
Ofisi ya Mkurugenzi, Halmashauri ya Manispaa Tabora, 4 Barabara ya Kiwanja cha Ndege
Anwani ya Posta: S.L.P 174, 45182 Tabora
Simu ya Ofisi: +255 262606088
Simu ya Mkononi: +255
Barua Pepe: md@taboramc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.