Na Paul Kasembo-TMC
Baraza la Waheshimiwa Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limeketi kwa siku mbili kupokea , kujadili na kupitisha taarifa mbalimbali robo ya pili (Oktoba – Desemba) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kutoka kwenye Kata na Kamati za Kudumu huku Baraza likiagiza utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa ili kuifanya Manispaa ifikie malengo iliyojiwekea ikiwamo kutoa huduma bora kwa wananchi wa Manispaa ya Tabora.
Akifungua mkutano huo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela alitumia fulsa hiyo kwanza kuwaomba wajumbe na wageni waalikwa kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kutoa heshima ya kumuombea kwa Mwenyezi Mungu pumziko la amani aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Magufuli ambaye ametimiza mwaka mmoja sasa tangu kufariki.
Kisha Mstahiki Meya alimpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea na utekelezaji wa maono yake yenye nia njema ya kuiondoa Nchi ilipo na kuipeleka kwenye uchumi wa juu zaidi.
Na kwa upande wa Manispaa ya Tabora, Baraza la Madiwani linamuombea kwa Mungu afya njema na kwa Baraza linaunga mkono juhudi zake zote pia lipo nyuma yake kumsaidia ili kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.
Mstahiki Meya alitumia fulsa hiyo pia kumshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Yahaya Nawanda kwa namna ambavyo anafanya kazi zake kwa juhudi kubwa sana kuwatumikia wananchi wake na hata anavyoisadia Manispaa ya Tabora kwenye ukusanyaji mapato ulinzi na usalama na hata anavyojitoa kwa dhati kabisa kuipaisha Manispaa ya Tabora kufikia lengo lake.
Baada ya kupokea taarifa zote kutoka kwenye Kata na baadae kutoka kwenye Kamati za Kudumu, Mstahiki Meya alimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Tabora ili aweze kutoa salamu za Serikali ya Wilaya ya Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Yahaya Nawanda aliwashukuru wajumbe wote kwa muitikio wao, akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipaisha Nchi yetu kimataifa, na kuendelea kuikumbuka Wilaya ya Tabora kwa kuleta miradi ya maendeleo yenye zaidi ya Bilioni 8 ndani ya mwaka mmoja.
Aidha aliwaeleza Wakuu wa Idara, Vitengo, Watendaji na watumishi wote wa Manispaa ya Tabora kutumia elimu zao walizosomea kutafisiri kwa vitendo ili kuweza kubadilisha maisha ya watu wa Wilaya ya Tabora kiuchumi, ustawi wa maisha, kuboresha mifumo yenye kuleta maisha bora kwa wananchi na siyo vinginevyo.
“Nawapenda sana Watumishi wenzangu, lakini sasa tuvae viatu ambavyo vinatutosha, nina maana kuwa msituangushe kwenye utekelezaji wa shughuri zenu za kila siku, mkafanye kazi kwa weledi kuiletea mafanikio chanya Manispaa ya Tabora,” alisema Dkt. Nawanda.
Akifunga mkutano, Mstahiki Meya alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa yote aliyoelekeza wameyapokea na kwamba watayafanyia kazi, na kwamba Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Tabora wanampenda sana na wanamuunga mkono kwa kazi zake zote na juhudi zake wanaungana nae.
Kisha akatumia fulsa hiyo kuwakumbusha Waheshimiwa Madiwani kwenda kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wao juu ya zoezi linaloendelea kwenye maeneo ya la Anwani za Makazi na Postikodi.
Twendeni tukawapatie ushirikiano wa kutosha wataalamu mtakaokuwa mnawaona wanafika kwenye maeneo yenu ili kuwezesha jambo hilo kutekelezeka kama lilivyokusudiwa, na Serikali sasa iweze kufanya upande wake wa kuwaletea maendeleo chanya wananchi wetu.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.