Na Alex Siriyako,
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa pamoja limetoa tamko la kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Samia Suruhu Hassani katika jitihada zake dhidi ya gonjwa hatari la UVIKO-19, pamoja na jitihada zake za dhati za kuleta maendelea kwa Watanzania hususani wakazi wa wilaya ya Tabora.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mh.Ramadhani Kapera ametoa tamko hilo kwa niaba ya madiwani wote na kusema kuwa kama wakazi wa Wilaya ya Tabora wanatoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kutupatia zaidi ya bilioni moja,milioni mia saba na thelathini kwa ajiri ya miradi ya sekta ya afya na elimu. Fedha hizo ni kwa mchanganuo wa bilioni moja na milioni mia mbili kwaajili ya madarasa idara ya elimu sekondari, milioni mia mbili na themanini kwa ajili ya madarasa ya shule shikizi za msingi,na milioni mia mbili na hamsini kwaajili ya kituo cha afya.
Baraza hili pia limepata kuhudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Dr.Batilda Buriani,Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora,Ndg.Ramadhani Katete,Mkuu wa Wilaya ya Tabora,Dr.Yahaya Nawanda, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wakuu wa taasisi za TUWASA,TANESCO pamoja na NMB tawi la Tabora. Pia watendaji mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora walihudhuria.
Baraza hili vilevile limejadili masuala mbalimbali yanayoihusu Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikiwa ni pamoja na taarifa za maendeleo za kata ishirini na tisa(29) za Manispaa, mwenendo wa mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ambapo mpaka sasa mapato yamefikia asilimia thelathini na sita (36%) ya makadirio yake ya mwaka. Lakini pamoja na yote baraza limeazimia ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba Halmashauri iwe imeshafikia asilimia hamsini ya makusanyo ya makadirio yake ya mapato na matumizi ya mwaka.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akiwa Mgeni mwalikwa katika Baraza hili,nae alipata fursa ya kuzungumza na Baraza na aliweza kumshukuru Raisi Samia Suruhu Hassani kwa kutupatia kiasi cha zaidi ya 1.7 bilioni kwa muda wa miezi mitatu,alipongeza sana umoja na mshikamano wa viongozi wakuu watatu wa Wilaya ambao ni Mkuu wa Wilaya,Meya wa Manispaa,pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora na kuongeza kuwa umoja wao ni mfano wa kuigwa na ndio chachu kubwa ya mafanikio ya Halmashauri ya Tabora. Ameipongeza pia Halmashauri kwa jitihada za kukusanya mapato na kuwasihi wasibweteke bali waongeze jitihada zaidi.
Pia Dr.Buriani ametahadharisha umuhimu wa kuzitumia nvua chache zinazotabiliwa mwaka huu na kuzingatia mazao yanayositahimili ukame kama alizeti. Vilevile Dr.Buriani ameipongeza Manispaa ya Tabora kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye mikopo ya vikundi vya vijana na walemavu. Hali kadhalika ametoa rai na kusisitiza suala la kuwapatia vizimba machinga litekelezwe kwa umakini mkubwa sana na kuongeza kwamba Manispaa ya Tabora haina budi kujifunza kwa halmashauri zingine zinafanya nini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,Dr.Peter Nyanja pamoja na mambo mengi aliyozungumza,ameahidi kuendeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo sio tu inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu bali na ile inayotekelezwa kwa mapato ya ndani, na kwa kuzingatia hilo ameshapeleka takribani asilimia ishirini ya mapato ya ndani kwenda kwenye miradi ya maendeleo hususani sekta ya Elimu Msingi ,Elimu Sekondari,Idara ya Kilimo na Mifugo pamoja na idara ya Maendeleo ya Jamii. Vilevile Dr.Nyanja ameahidi kuendeleza jitihada za kukusanya mapato na atashughulikia suala la Machinga kwa umakini na weledi mkubwa.
Katika kuhitimisha kikao cha Braza la Madiwani,Mstahiki Meya ametoa taarifa kuwa Halmashauri itaajili vijana takribani thelathini ili kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Amesisitiza pia suala la umoja wa watendaji kata,madiwani ,wakuu wa shule na Madaktari katika kutekeleza ujenzi wa miradi inayoendelea . Vilevile ametoa rai kwa Mkurugenzi kuwa makini sana katika ugawaji wa vizimba kwa machinga na kusisitiza wauzaji wa mbogamboga walioko pembezoni mwa barabara hawana bdi kwenda kwenye masoko kwani kule nafasi ziko nyingi na ziko wazi
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.