Na Alex Sriyako-TMC
Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela wametoa pongezi zao za dhati kabisa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter M. Nyanja na Menejimenti yote kwa ujumla kwa kasi yake ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ambapo kwa kipindi cha Julai-Septemba 2022/2023 Halmashauri imekusanya asilimia 32.15, na mpaka kikao cha robo ya kwanza kinafanyika mnamo tarehe 2.11.2022 makusanyo yako asilimia 43.59, kasi amabayo inaridhisha sana.
Wajumbe wa Baraza wamempongeza Mkurugenzi na kuongeza kuwa kwa Manispaa ya Tabora kwa miaka ya hivi karibuni hawajawahi kuona kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kiwango hiki. Wajumbe wamesisitiza jitihada hizi za makusanyo ni za kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani uhai wa Halmashauri ni mapato.
Aidha Mstahiki Meya katika hotuba yake ya ufunguzi amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi sana za miradi katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora hususani Sekta ya Elimu ambayo ndiyo roho ya uchumi endelevu wa Taifa, na akakumbusha tu kuwa katika kipindi cha Julai-Septemba miongoni mwa fedha sekta ya Elimu imepokea, Halmashauri imepokea kiasi cha Bilioni moja ,milioni miatatu na themanini (1,380,000,000) kwaajili ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Baraza wametoa tuzo ya Ngao kwa Wananchi wawili wa Manispaa ya Tabora kwa kuonyesha uzalendo mkubwa na wa kuigwa wa kutoa maeneo yao kupisha ujenzi wa miundombinu ya Elimu. Wananchi hao ni Mhe. Mohamed Katete, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora ambaye ametoa eneo lake ili ijengwe Shule ya Msingi katika Kata ya Ipuli, pamoja na Ndugu Idd Rajabu ambae ametoa eneo ilipojengwa Shule ya Sekondari Mpera, kata ya Mpera. Wajumbe waliongeza msisitizo kuwa Shule ya Msingi inayojengwa isajiliwe kwa jina la Mzee Katete ili kuenzi mchango wake katika jamii na kwa upande wa Ndugu Rajabu apewe jina la Mtaa kwasababu Shule ya Mpera imeshasajiliwa kwa jina tofauti.
Katika Baraza hili vilevile kumeibuka hoja za utekelezaji usiolizisha wa Shirika la Umeme Nchini(Tanesco) Mkoa wa Tabora hususani kwenye kasi yao ya kupeleka umeme vijijini. Hata hivyo wajumbe wameishia kumuagiza mwakilishi wa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tabora baada ya Meneja kuwa na udhuru na kushindwa kuhudhuria Baraza hili. Aidha Wajumbe wameliomba Shirika la Umeme Mkoani Tabora lirudishe umeme katika chanzo cha Uzalishaji wa Maji cha Mto Igombe ambacho kipo chini ya Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Mkoani Tabora (TUWASA) ili Wananchi waendelee kupata huduma ya maji na kuongeza kuwa changamoto zingine zitatuliwe kiofisi.
Msathiki Meya wa Manispaa ya Tabora katika kuhitimisha Baraza hili amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kuendeleza kasi yake ya kukusanya mapato kwa kushirikiana na wadau wake wote na ajitahidi kusikiliza kero zao.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.