Mheshimiwa Ramadhani Kapela, ambae ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ameongoza kikao cha Baraza la Waheshimiwa Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Baraza hilo vilevile limehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Wilaya ya Tabora, Ndg.Mohamed Katete, Mkuu wa wilaya ya Tabora, Dkt. Yahaya Nawanda, Mkurugezi wa Manispaa ya Tabora,Dkt Peter Nyanja, Katibu tawala wa Wilaya ya Tabora, Ndg.Hamarskjold Yonaza, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Ndg. Sefu Salum,Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Waheshimiwa madiwani, Watendaji wa serikali, pamoja na wageni waalikwa.
Mstahiki Meya alifungua kikao hicho mahususi kwa ajili ya maamuzi na ustawi wa maendeleo ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na aliwakaribisha Mkuu wa wilaya Yahya Ismail Nawanda katika baraza lake la kwanza na Mkurugezi mpya Dkt Peter Maiga Nyanja. Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt Batilda Burian, kwa kazi zake nzuri na alimshukuru Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu kwa uongozi wake mzuri na vilevile alishukuru kwa ushirikiano anaopata kutoka kwa madiwani.
Mheshimiwa Ramadhani alisisitiza hatua za dhati zichukuliwe kuinua mapato, asilimia za maendeleo kutoka kwenye makusanyo ziende kwa wananchi kwa wakati, na zaidi ya yote akasisitiza viongozi wa serikali lazima wawe mstari wa mbele kuhamasisha zoezi la chanjo za UVIKO-19.
Dkt.Peter Nyanja, yeye aliomba ushirikiano kutoka kwa madiwani pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama hususani kwenye kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, kwani anaamini kuna uwezekano mkubwa wa kufikia asilimia mia moja, ikiwa ni pamoja na kusuluhisha matatizo madogo madogo ya ulipaji kodi, pia aliomba kuungwa mkono katika uimarishaji wa usafi wa mji na kusisitiza biashara holela zipigwe marufuku kwamba kila biashara ina sehemu yake stahiki na kodi stahiki za Halmashauri lazima zilipwe.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt.Yahaya Nawanda, naye alipata fursa ya kuzungumza machache, ambapo alimshukuru Rais kwa kuendelea kumuamini katika nafasi hiyo, aliahidi ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya. Alisema hatokubali Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuwa ya mwisho kwenye mapato, na zaidi ya yote alitoa rai kwa matumizi sahihi ya fedha zinazokusanya, ikiwa ni sambamba na uwepo wa nyaraka zote za manunuzi, na matumizi mengineyo.
Miongoni mwa matukio yaliyofanyika ndani ya vikao hivi ni pamoja na kuzitambua na kuzitunuku vyeti shule za Msingi na Sekondari za Tabora Manispaa, zilizofanya vizuri katika mitihani ya Taifa kwa mwaka 2020, Kumtambua na kumpongeza mwanafunzi Bora Hassan wa Shule ya Sekondari Nyamwezi kwa kutwaa nishani nne katika michuano ya UMISETA ngazi ya Taifa. Hali kadhalika, Baraza limepokea ripoti ya Mpango kazi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kutoka Shirika la umeme TANESCO, pamoja na TARURA
Baraza vilevile ndani ya vikao vyake vya siku mbili limeweza kupata fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa Meya, limepokea taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kila kata, limepokea Mihutasari na maadhimio ya Kamati mbalimbali za kudumu, Lakini vilevile Baraza limepokea taarifa ya Mkaguzi wa Ndani kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Kabla ya kufunga kikao, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora, Ndg. Mohamed Katete, alimpongeza mwenyekiti wa kikao, Mh.Ramadhani Kapela kwa kuonyesha umahiri wake na kuweza kuwaunganisha Watendaji wa Serikali na Waheshimiwa Madiwani. Hali kadhalika, Ndg.Katete alisema kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ina mipango mingi mikubwa ila haijatekelezwa kwa sababu ya changamoto kama vile ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji, hivyo aliwaasa viongozi kubadirika na kufanya kazi kwa bidii na kuwa wavumilivu na kuwa watunzaji wa kumbukumbu na nyaraka muhimu za Serikali.
Mwenyekiti wa kikao ambae ni Meya wa Manispaa ya Tabora, Mh. Ramadhani Kapela alifunga kikao hicho kwa kumshuru Mungu kwa uzima, uhai, hekima na busara kwa kumaliza kikao hicho salama, pia alishukuru kwa ushirikiano mkubwa kutoka Waheshimiwa Madiwani. Hali kadhalika, Meya alisisitiza Viongozi wa Serikali kuwa mstari wa mbele kuhamasisha chanjo, na alitanabaisha kwa mara nyingine kwamba kipaumbele cha Baraza la Madiwani ni kuongeza Mapato kadri itakavyowezekana.
Mwisho.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.