Na Alex Siriyako,
Mzee Joseph Rutambuka mwenye umri wa miaka 65 mpaka sasa, ni mkazi wa Kata ya Mtendeni iliyopo manispaa ya Tabora,ambae mpaka sasa ameweza kuishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa zaidi ya miaka kumi na sita . Mzee Rutambuka alibainika na maambukizi ya VVU kwa mara ya kwanza mwaka 2005.Anaeleza kuwa siri ya mafanikio yake ni matumizi mazuri ya dawa za kupunguza makari ya Virusi pamoja na kufuata ushauri mwingine wa madaktari kama kula vizuri,kuepuka ngono uzembe,kufanya mazoezi pamoja na kujiamini na kuwa mwenye furaha muda mwingi.
Mzee Joseph Rutambuka ni miongoni mwa mashujaa wa siku ya UKIMWI DUNIANI,kwani ni miongoni mwa waathirika wachache sana Nchini Tanzania ambao wamejitokeza hadharani na kuieleza jamii kwamba wao ni wahanga wa VVU.Mzee anaishi na maambukizi na sasa amekuja kuwaelimisha wakazi wa Itulu,na kuwatia moyo wale wenye maambukizi kwamba wasikate tama kwani inawezekana kuishi na maambukizi na ukafikia ndoto zako.
Pamoja na mafanikio hayo vilevile Mzee Rutambuka anaeleza changamoto ambazo amekutana nazo ikiwa ni pamoja na kupoteza wanafamilia ambao ni mke na mtoto mmoja. Vilevile amenyanyapaliwa sana na jamii pindi alipobainika anamaambukizi ya UKIMWI. Lakini amepambana na changamoto hizo na anawaasa wanajamii waweze kuchukua hatua dhidi ya gonjwa hili ikiwa ni pamoja na kupima mara kwa mara ,Kuchukua dawa za kupunguza makari ya Virusi mapema pindi wanapobainika kuwa na VVU ,pamoja na kuwapenda wenye VVU na kuwafariji badala ya kuwanyanyapaa.
Katika maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI DUNIANI ambayo kitaifa yaliadhimishwa Mkoani Mbeya, kwa Wilaya ya Tabora yalifanyika kijiji cha Itulu,kata ya Ndevelwa. Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mh.Dkt.Ismail Yahaya Nawanda ambae alipata wasaa wa kuongea na Wananchi wa Itulu. Dkt.Nawanda alieleza vizuri kuwa malengo mahsusi ya Siku ya UKIMWI Duniani ni kuwakumbuka wapendwa waliotutoka kwa sababu ya janga hili,lakini pia ni kupata fursa ya kukumbushana kuwa UKIMWI bado upo na unaendelea kututafuna taratibu na hivyo hatuna budi kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kuendelea kupambana ili hatimae tuweze kulitokomeza janga hili.
Dkt.Nawanda ameeleza mikakati ya Serikali katika kupambana na janga hili ni pamoja na kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanafikia sifuri,Unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU unakwisha, pamoja na kuhakikisha kwamba vifo vitokanavyo na UKIMWI vinakwisha kwa kuendelea kutoa elimu kwa wadau wote.
Lakini pia Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa Wananchi kijitokeza kupima kwa hiari ili kujua afya zao, akinababa waende na kina mama kiliniki ili kujua afya zao na kuweza kumkinga mtoto na maambukizi ya VVU. Pia alitoa wito kwa wadau kupata chanjo ya UVIKO-19, kwani CORONA ipo na inaua,njia pekee ya mwisho kukabiliana nayo kwa sasa ni chanjo. Dkt.Nawanda alimaliza kwa kusema “Tabora Manispaa bila maambukizi mapya ya UKIMWI inawezekana”
Bi.Aziza Mageta,ambae ni Mratibu wa UKIMWI katika Manispaa ya Tabora,katika risala yake fupi ameeleza Historia ya Gonjwa la UKIMWI kwa ufupi sana. Ameeleza kuwa ugonjwa huu uligundulika kwa mara ya kwanza Nchini Marekani mnamo mwaka 1981,na kwa Tanzania ugonjwa huu ulionekana Mkoani Kagera mwaka 1983, na mnamo mwaka 1984 ugonjwa huu ulikuwa umeingia Mkoani Tabora. Alieleza pia mnamo mwaka 1985 mgonjwa wa kwanza alilipotiwa ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Lakini vilevile Bi.Aziza ameeleza namna ambavyo wakazi wa Tabora wanahitaji kuchukua tahadhari zaidi kwani hali ya maambukizi kwa Wilaya yetu sio nzuri, kwani kwa mwaka 2019/2020 kiwango cha maambukizi kilikuwa 3.5, na kwa mwaka 2020/2021 kiwango cha maambukizi ni 3.8 hali ambayo ni ya hatari sana kwani maambuklizi yameeongezeka kwa asilimia tatu(3%). Hivyo amewaomba Wananchi wote wa Tabora tutambue hali hii na tuongeze jitihada katika kupambana na janga hili.
Miongoni mwa wadau waliofika katika kuadhimisha siku hii ya UKIMWI DUNIANI katika Kijiji cha Itulu,Kata ya Ndevelwa Wilayani Tabora ni pamoja na DAMU SALAMA kanda ya Magharibi,EWURA-CCC, Shirika risilo la Kiserikali la COMPASSION, Mpango wa TOHARA, pamoja na Wataalamu wa Wizara ya Afya wa Chanjo ya UVIKO-19, na Upimaji wa VVU. Vilevile Wananchi wa kata ya Ndevelwa walihudhuria kwa wingi wao.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.