Na Alex Siriyako,
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Raisi,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mh.Ummy Mwalimu amepiga marufuku michango yeyote isiyofuata utaratibu katika shule zote za Sekondari na Msingi.Waziri Ummy ametoa onyo hili katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora,katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Na katika msisitizo wa onyo hilo,Waziri ametoa Salamu za Mh.Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mama Samia Suruhu Hassani kwa WanaTabora,kwamba Mh.Raisi ataendelea kutoa fedha za Elimu bure, hivyo Wananchi wapuuze taarifa zinazosambaa za kulipa ada Mashuleni.
Waziri Ummy amekagua Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Miongoni mwa miradi aliyopata fursa ya kutembelea na kukagua ni pamoja na; Ujenzi wa Madarasa mawili na Ofisi moja katika Shule ya Sekondari Kariakoo. Mh.Ummy ameridhika na ubora wa madarasa na kwa kuthibitisha hilo ameahidi kuleta milioni hamsini(50,000,000/=) za kujenga Jengo la Utawala shule ya Sekondari Kariakoo.Lakini vilevile alitumia wasaa huo kukanya na kuonya juu ya michango isiyofuata taratibu za kisheria na kusema kwamba michango yote ya shule kwanza lazima ijadiliwe na kukubaliwa na bodi ya shule kabla ya Vyombo vingine vya Serikali.
Mh.Ummy aliweza kukagua Kikundi cha Vijana cha Miombo Bee Keepers Initiatives, Kikundi cha Vijana kinachojihusisha na Ufugaji Nyuki na Kusindika Mazao ya Nyuki.Kikundi hiki ni miongoni mwa Vikundi vilivyopata mkopo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkopo wa kiasi cha shilingi Milioni Hamsini(50,000,000/=),ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Raisi kwa Halmashauri zote Nchini kutoa mikopo yenye tija kwenye vikundi vya wajasiriamali,badala ya mikopo ya pesa ndogo ndogo,ambayo haiwainui vijana ipasavyo.
Halikadhalika Mh.Ummy amekagua Ujenzi wa Haspitali ya Wilaya ya Tabora,ambapo ameridhika na ubora wa Majengo lakini pia ametoa maagizo Halmashauri ifanye hima iweze kumaliza ujenzi huo ili Wananchi waanze kupata huduma, vile vile amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dr.Peter Nyanja,aanze kujenga nyumba za watumishi kwa mapato ya ndani.
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI amekagua ujenzi wa Barabara ya Milambo Barracks, barabara yenye urefu wa Mita mia nane inayojengwa kwa kiwango cha rami kwa kutumia fedha za Serikali na inatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni miatatu ishirini mpaka kukamilika.Mh.Ummy ameridhika na kasi ya ujenzi na kuhimiza mradi umalizike kwa wakati.
Waziri Ummy anaendele na Ziara yake Mkoani Tabora, kwa Upande wa Halmashauri ya Manispaa yaTabora ,amempongeza kwanza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt.Batilda Buriani, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt.Yahaya Nawanda pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa usimamizi wao mzuri wa miradi ya maendeleo hususani utekelezaji wa ujenzi wa madarasa 74 ya Mpango wa Taifa wa Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.