Na Alex Siriyako;
Wataalamu wa Manispaa ya Tabora ambao ni Wakuu wa Divisheni na Vitengo wenye kusimamia vyanzo vya Mapato wamesainishwa Mikataba ya kuhakikisha kuwa wanafikia malengo ya ukusanywaji wa mapato katika vyanzo wanavyovisimamia kwa asilimia mia moja ama zaidi kwa kadri ya makisio ya bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mikataba hiyo imesainiwa leo Julai 10,2023 baina ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndugu Elias M. Kayandabila na Wakuu wa Sehemu na Vitengo wenye Vyanzo vya Mapato ambavyo wanavisimamia katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora huku zoezi hili likishuhudiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela.
Akieleza kikao kabla ya utiaji saini huu, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora ameeleza kuwa Bajeti ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni bilioni 6.15 ambazo zinatokana na vyanzo vingi ambavyo vinasimamiwa na Wakuu wa Sehemu na Vitengo tofauti tofauti.
Mkurugenzi ameongeza kuwa ili kufanikisha zoezi la kukusanya Mapato ya ndani kwa ufanisi, Wakuu wa Sehemu na Vitengo hawana budi kusimamia vyema na kwa weledi na uaminifu vyanzo vilivyo chini yao na kuhakikisha kuwa makisio waliyokadiria kwenye vyanzo hivyo yanakusanywa ipasavyo.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela kwa nafasi yake amempongeza Mkurugenzi kwa jitihada zake za awali za kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri yanapatikana kwani mapato ndio roho ya Halmashauri yeyote ile Duniani.
Mhe. Kapela ameongeza kuwa ana imani kubwa sana na Wakuu wa Sehemu na Vitengo waliopo kwani kwa miaka miwili ya fedha iliyopita wamefanya kazi nzuri ya makusanyo ya mapato ya ndani ikiwa ni sambamba na kuzifanyia kazi hoja za ukaguzi na kupata hati safi kwa miaka miwili hiyo mfululizo.
Hivyo Mstahiki Meya amewataka Wakuu wa Sehemu na Vitengo wasiwe na wasiwasi na Mikataba hii kwani ina lengo zuri sana la kuongeza tija na ufanisi kwa mtu mmoja mmoja kama Kiongozi katika usimamizi wa chanzo ama vyanzo vilivyo chini yake na ameongeza kuwa atafurahi sana kama kutakuwa na bonasi kwa Mkuu wa Sehemu ama Kitengo atakaye kusanya zaidi ya asilimia mia moja.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.