Na Alex Siriyako:
Wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma Tanzania (PPRA) Kanda ya Magharibi na Kati wakiongozwa na Kaimu Meneja wa Kanda hii Mhandisi Suma Atupele, wametembelea Halmashauri ya Manispaa ya Tabora leo Aprili 5,2024, ambapo wamekutana na kuzungumza na Wakuu wa Sehemu na Vitengo. Aidha Mhandisi Atupele ameongozana na Bi. Anna Bubele ambaye ni Afisa Manunuzi pamoja na Ndugu Jumanne Marumbo ambae ni Mkadiriaji Majenzi.
Katika ujumbe wake mfupi Mhandisi Atupele amefafanua kuwa, zaira yao katika Manispaa ya Tabora pamoja na mambo mengine ni kujitambulisha, kwa kutambua kuwa ofisi za PPRA Kanda ya Magharibi na Kati ndio zimefunguliwa hivi karibuni, amehimiza matumizi ya mfumo wa manunuzi wa sasa yaani NeST( National e-Procurement System of Tanzania) katika manunuzi ya Serikali ya aina yeyote na zaidi amewakumbusha Wataalamu kuendelea kusimamia vyema fedha za miradi kwenye taasisi zilizo chini yao na katika hili amesisitiza Wahandisi wafike saiti mara kwa mara kutoa maelekezo na kuepuka makosa yanayowezekana kuepukika.
Kwa upande wao Wataalamu wa Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mhifadhi Sefu Salumu (Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora), wameeleza changamoto wanazokabilina nazo katika matumizi ya mfumo wa manunuzi wa sasa (NeST).
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na miradi kuchelewa kukamilika kwasababu ya taratibu za mfumo wa NeST kuchukua muda mrefu, wazabuni kupandisha bei za bidhaa na vifaa vya ujenzi kwa madai kuwa kuna gharama wanazolipa kujisajili kwenye mfumo huu wa NeST, na wakaongeza kuwa utaratibu wa manunuzi ya Manispaa yote kufanyika kwenye ofisi ya Manunuzi ya Manispaa nayo ni sababu ya kupoteza muda wa kutekeleza miradi na katika hili wameshauri PPRA iangalie namna bora ya kuwapa elimu Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule ,Waganga Wafawidhi pamoja na wazabuni, lengo likiwa kupata uelewa wa kutosha kuhusu mfumo huu na faida zake, lakini pia kuweza kuondoa baadhi ya vikwazo katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Mhandsi Atupele katika kutolea ufafanuzi hoja zilizotolewa amefafanua kuwa kwa sasa PPRA kwa kushirikiana na TAMISEMI wameshakamilisha mfumo wa manunuzi kwenye ngazi za vituo vya kutolea huduma za afya na mashule na kilichobaki ni mafunzo tu ili mfumo huo uanze kutumika.
Aidha amefafanua kuwa hakuna sababu yeyote ya bei za vifaa vya ujenzi kupanda bei kwa kuzingatia kuwa asilimia kubwa ya fedha zote za miradi ya maendeleo ngazi ya chini hazina kodi (VAT exclussive), na akaongeza kuwa labda kinachohitajika kwa sasa ni elimu itolewe ya kutosha kwa wazabuni.
Mhandisi Atupele amefafanua kuwa mfumo wa manunuzi wa sasa (NeST) hausababishi manunuzi kuchelewa kwa namna yeyote ile kwani zabuni ikishatangazwa ni jukumu la Afisa Manunuzi kufuatilia zabuni hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapa taarifa wazabuni wake wa karibu kama mafundi ujenzi ili waweze kuomba, na katika hili ametolea mfano kuwa PPRA iliamua kupunguza vigezo kwa mafundi ujenzi (Local Fundi) ili tu kutokuathiri namna kazi za ujenzi kwa mfumo wa FORCE ACCOUNT zinavyofanyika.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.