Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Mhe. Ramadhan Kapela ametoa wito kwa wakazi wa Tabora kuilinda na kuitunza miundombinu inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya TACTIC, ili kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa na tija ya muda mrefu kwa wananchi.
Mhe. Kapela alisema hayo wakati wa Hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kituo cha Mabasi eneo la Inala pamoja na Ujenzi wa soko la Mjini Kati kupitia mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (TACTIC) katika Manispaa ya Tabora leo Disemba 05, 2024
“Miradi hii tumeisubiri kwa hamu kubwa na ni jambo la kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza kiu ya wanatabora, rai yangu ni kuipokea miradi hii na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu na kuleta tija,” alisema Mhe. Kapela.
Aidha, Mhe. Kapela ametoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazokuja wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Manispaa ya Tabora ili kuweza kuitumia kama sehemu ya kujiingizia kipato binafsi na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Tabora.
Pia Mhe. Kapela ameshukuru ujio wa mradi huo wa TACTIC akisema unaenda kuchagiza adhma yao ya kuifanya Manispaa hiyo ya Tabora kuwa Jiji.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo ya TACTIC, Mhe. Kapela amemuahidi Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba kuwa watasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na thamani ya fedha ikionekana, akiwataka pia Vijana watakaopata fursa za ajira kwenye wakati wa ujenzi wa miradi hiyo kuwa waaminifu na kujiepusha na wizi wa vifaa vya ujenzi.
Mhe. Kapela amehimiza pia wananchi wa Taboa kuchangamkia fursa za ujio wa miradi hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanakuwa sehemu ya wanufaika wa vizimba na mabanda mbalimbali yatakayojengwa kwenye soko na kwenye kituo cha mabasi Inala.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.