Na Paul Kasembo-TMC
Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dkt. Yahaya Nawanda ametoa wito kwa Kamati ya Afya ya Masingi Tabora Manispaa na makundi mbalimbali wakiwemo na Wataalamu wa afya, Viongozi wa Dini, Waalimu, Viongozi wa Mitaa, Vijiji, Wakuu wa Taasisi na Ofisi nyingine za Serikali zilizopo hapa Tabora Mjini pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kushiriki kikamilifu katika Mpango Harakishi wa Utoaji Chanjo ya Uviko-19.
Dkt. Nawanda ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Kamati ya Afya ya Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Tabora uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa na kwajumuisha wadau mbalimbali wa afya.
“Kampeni hizi za chanjo zimekuwa zikifanyika Nchi nzima ni muendelezo ukizingatia kuwa Tanzania inaungana na Nchi nyingine kote Duniani kuhakikisha kuwa inapambana na ugonjwa huo na kuweka mikakati madhubuti wa kujikinga na UVIKO-19 ikiwa ni pamoja uimarishaji wa utoaji chanjo hiyo”, alisema Dkt. Nawanda.
Aidha Dkt. Nawanda alisema kuwa chanjo ya UVIKO-19 inatolewa kwa hiari kwenye maeneo zaidi ya 35 ndani ya Manispaa ya Tabora pamoja na huduma ya Vituo tembezi ambapo ambapo amewataka wadau wa kikao cha afya waende kuwa wawakilishi, wasaidie kutoa elimu kwa wananchi walioko kwenye maeneo na wakawe mabalozi wazuri huku wakitumia kauli mbiu “AFYA NI MTAJI, MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19 NI WAJIBU WETU TUJUMUIKE KWA PAMOJA, CHANJO NI SALAMA.”
Kando na Dkt. Nawanda, Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Tabora Ndg Vitus Ntenga alisema kuwa kirusi cha Korona ambacho ni kipya duniani, ni sehemu ya familia ya virusi vinavyosababisha homa ya mafua kwa miaka mingi, ambapo uzalishwaji wa chanjo ya UVIKO-19 umetokana na muendelezo wa tafiti zilizofanywa muda mrefu, jitihada za mataifa jumuishi pamoja na taasisi za utafiti wa magonjwa ya dharula na yale ya mlipuko.
Hitimisho la mkutano huo ambao ulijumuisha wadau mbalimbali limekubaliana kwa kauli moja kuwa kufikia lengo la kumaliza chanjo zilizopokelewa na kwa asilimia 100 kabla ya mwezi Novemba 2021.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.