Na Alex Siriyako,
Haya yamesemwa na Bi. Haika Masue, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora akimuwakilisha Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Paul Chacha katika kikao cha tathimini ya lishe Manispaa ya Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa leo tarehe ishirini na nane Oktoba.
Manispaa ya Tabora kupitia kwa Watendaji wake kama Maafisa Lishe na Watendaji Kata, inayo dhima na dhamana kubwa sana kuhakikisha kuwa Wananchi wake wanapata lishe bora na yenye virutubisho vyote muhimu kwa afya zao.
Bi. Haika amesisitiza kuwa Lishe duni sio tu inaathiri maendeleo ya mtoto lakini pia inaathiri ukuaji wake kimwili na kiakili na hatimaye kuathiri mchango wake katika maendeleo ya Taifa kipindi chote cha uhai wake.
Ametanabaisha kuwa hali ya Utapiamlo katika Mkoa wa Tabora ni kubwa hali ambayo ni mbaya Zaidi kwa watoto chini ya miaka mitano, wanawake wajawazito na akina mama wanaonyonyesha. Hali kadhalika amewaasa Wakazi wa Tabora kunawa mikono kwani afya bora huanzia kwenye usafi wa mwili ikiwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara.
Bi. Haika amewakumbusha Menejimenti ya Manispaa ya Tabora kuwa mnamo tarehe 30/9/2022 Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameingia Mkataba na Wakuu wa Mikoa yote Nchini ya uboreshaji wa shughuli za Lishe, Mkataba utakaodumu kwa miaka minne na umeainisha vipaumbele vyake pamoja na viashiria vya lishe. Hivyo Manispaa ya Tabora ina dhima na dhamana kubwa kufanya vizuri sana katika kutekeleza mkataba huu.
Hali kadhalika Wajumbe wa kikao hiki wakiongozwa na muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Tabora walishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Lishe baina ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora na Watendaji wa Kata 29 za Manispaa ya Tabora. Ambapo kwa mkataba huo, Watendaji Kata watahakikisha Wananchi kwenye Kata zao wanapata Vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu ili kuepuka utapiamlo.
Ndugu Sefu Salumu Sefu, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora naye amepata wasaa wa kuzungumza na wajumbe ambapo amepokea maelekezo yote ya Serikali na kusisitiza kuwa Menejimenti ya Manispaa ya Tabora ikiongozwa na Mkurugenzi wake itahakikisha mikataba ya lishe baina ya Mkurugenzi na Watendaji wa Kata inatekelezwa kwa asilimia zote.
Akifunga kikao hiki Bi. Haika amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kutunga Sheria Ndogo itakayosimamia utekelezaji wa shughuli za lishe. Pia amewataka Watendaji Kata kupata takwimu sahihi za hali ya lishe kwa maafisa lishe ngazi ya jamii ili ziwasaidie katika kupambana na lishe duni kwenye kata zao.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.