Na Alex Siriyako:
Madiwani ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Elimu na Afya katika Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hii Mhe. Salumu Msamazi ambae pia ni Diwani wa Kata ya Ikomwa wamemshauri Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kuangalia bajeti ya dharula kwaajili ya ujenzi wa vyoo katika baadhi ya Shule za Msingi za Manispaa ya Tabora ambazo vyoo vyake vimetitia, kubomoka na vingine kujaa maji kabisa kiasi haviwezi kutumika kufuatia mvua nyingi zinazonyesha msimu huu katika Manispaa ya Tabora na maeneo mengine ya Tanzania.
Ushauri na maelekezo haya yametolewa na Madiwani wa Kamati hii ya Uchumi, Elimu na Afya leo Februari 21,2023 wakiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Manispaa ya Tabora katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/20224.
Pamoja na mambo mengine, Waheshimiwa madiwani wameweza kutembelea na kuona umaliziaji wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Tabora iliyopo Kata ya Mpera, wameona uharibifu wa vyoo katika shule za Msingi Ulamba iliyopo Kata ya Kalunde, Shule ya Msingi Mawiti iliyopo Kata ya Malolo, Shule ya Msingi Chemchem iliyopo kata ya Chemchem, pamoja na Shule ya Msingi Masubi iliyopo Kata ya Cheyo.
Aidha Mheshimiwa Salumu Msamazi kwa niaba ya wajumbe wa Kamati amemshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za maendeleo ambazo anaendelea kuipatia Manispaa ya Tabora, lakini pia akasisitiza Menejimenti ya Manispaa ya Tabora kusimamia ipasavyo fedha za miradi, lakini pia ihakikishe inatatua kero ya vyoo vyenye hali mbaya sana katika shule za Msingi zilizoathiriwa na mvua nyingi za msimu huu.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.