Na Alex Siriyako:
Miradi sita yenye thamani ya Zaidi ya bilioni 2.5 katika Wilaya ya Tabora imepata Baraka za Viongozi wakimbiza Mwenge Kitaifa wanaoongozwa na Kiongozi wao Ndugu Abdallah Shaibu Kaim.
Mwenge wa Uhuru umepokelewa leo Septemba 15, 2023 katika viwanja wa shule ya Sekondari Itetemia, Wilaya ya Tabora ukitokea Wilaya ya Sikonge ambapo umetembelea na kukagua miradi sita katika sekta ya Maji, Afya, Maendeleo ya Jamii, Elimu pamoja na Hifadhi ya Mazingira.
Miradi hii ambayo imetembelewa na kukaguliwa na Viongozi wakimbiza Mwenge Kitaifa katika Wilaya ya Tabora ni pamoja na mradi wa maji safi uliopo Kata ya Ntalikwa , Kitengo cha kusafisha figo ( Dialyis) katika Hospitali ya Malolo iliyopo Kata ya Malolo, Kikundi cha Bright Vision ambacho kinafanya kazi ya kufyatua tofari ambacho kipo kata ya Mbugani na ni miongoni mwa vikundi vinavyonufaika na Mkopo wa Halmashauri wa 10% na kimeshakopeshwa mkopo wa milioni ishirini, Mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na Ofisi moja katika Shule ya Bombamzinga iliyopo Kata ya Isevya, Mradi wa barabara ya Warangi yenye urefu wa mita 1800 kwa kiwango cha rami na mradi wa mwisho ni mradi wa upandaji miti 1000 shule ya msingi Manoleo iliyopo kata ya Itonjanda.
Hivyo basi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Ndugu Abdalah Shaib Kaim ameweka jiwe la msingi katika mradi wa maji safi Kata ya Itonjanda, amezindua mradi wa huduma ya kusafisha figo ( DIALYSIS) uliopo Hospitali ya Malolo katika kata ya Malolo, ametembelea na kukagua kikundi cha Bright Vision kinachofyatua tofari , amezindua jengo la madarasa mawili na ofisi moja katika shule ya msingi Bombamzinga, Kata ya Isevya, ameweka jiwe la msingi mradi wa barabara ya Warangi iliyopo Kata ya Mpera na mwisho kabisa ametembelea mradi wa upandaji miti uliopo shule ya msingi Manoleo Kata ya Itonjanda.
Aidha, Ndugu Abdalah Shaibu Kaim katika ujumbe wake wa Mwenge wa Uhuru kwa Wakazi wa Wilaya ya Tabora amesisitiza jamii kuweka mkazo, kuzingatia na kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya Rushwa, Madawa ya Kulevya, Ugonjwa wa Malaria, Maambukizi mapya ya VVU na ugonjwa wa UKIMWI, na kuzingatia uraji wa lishe bora katika maisha yetu ya kila siku.
Vilevile Ndugu Abdalah ameeleza kwa kina sana juu ya umuhimu wa Watanzania kuweka kipaumbele suala la athari za kimazingira zinazotuathiri kila siku kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo chanzo kikubwa ni uharibifu wa mazingira kwa shughuli zetu za kibinadamu za kila siku kama kilimo pembezoni mwa vyanzo vya maji, ufyekaji misitu hovyo, ufugaji wa mifugo mingi kihorela bila kufuata taratibu na kanuni za ufugaji bora na salama.
Hivyo ameiasa sana Jamii ya Wakazi wa Tabora na Tanzania kwa ujumla kuzingatia umbali wa vyanzo vya maji kwenye shughuli za kilimo, kuzingatia ufugaji bora unaofuata kanuni, lakini pia na kutunza misitu yetu ya asili ikiwa sambamba na kutekeleza maagizo ya Serikali ya kupanda miti kwa wingi na hasa amezikumbusha Halmashauri jukumu la kupanda miti milioni moja na nusu kila mwaka.
Ndugu Abdalah kwa niaba ya Wakimbiza Mwenge Kitaifa wengine alioambatana nao, amewashukuru sana wakazi wa Wilaya ya Tabora kwa kujitokeza kwa wingi kuja kuupokea Mwenge wa Uhuru na amefurahishwa sana na mapokezi mazuri amabyo vilevile yameenda sambamba na miradi mizuri.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.