Na Alex Siriyako:
Mashindano ya UMITASHUMTA Kitaifa ambayo yamedumu kwa takribani Wiki mbili kuanzia Juni 3,2023 hapa Mkoani Tabora katika viwanja vya Tabora Boys na Tabora Girls yakishindanisha timu kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani yamefikia tamati leo hii Juni 13,2023.
Akifunga Mashindano haya Naibu Waziri ,Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuziwezesha Wizara tano ambazo zimehusika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mashindano haya ambazo ni Wizara ya Fedha na Mipango, TAMISEMI, Elimu ,Sayansi na Teknolojia,Utamaduni ,Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amari ya Zanzibar.
Aidha Waziri Kipanga amewapongeza kwa dhati kabisa Uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa maandalizi mazuri ya michezo hii lakini vilevile kwa kusimamia vyema sana ulinzi wa watoto hawa kwa muda wote ambao wamekuwa hapa Mkoani Tabora.
Waziri Kipanga ameelekeza kuwa michezo,Sanaa na ubunifu ipewe kipaumbele mashuleni kwani huleta tija kubwa sana na kuleta matokeo chanya kwenye ujifunzaji shuleni na vyuoni.
Mhe. Kipanga ameeleza kuwa Rasmu ya Maboresho ya Mitaala ya mwaka 2023 imeongeza michepuo ya Sanaa, michezo na mziki lengo ikiwa ni kuendeleza vipaji vya wanafunzi na kuwawezesha kutumia vyema sana vipaji vyao katika maisha yao.
Michezo hii imekamilika kwa ngazi ya UMITASHUMTA Kitaifa huku Mkoa wa Mwanza ukiibuka kidedea kwa kubeba vikombe vingi, lakini pia ukishika nafasi ya kwanza Kitaifa kwa ushindi wa jumla.
Mwisho
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.