Na Alex Siriyako;
Manispaa ya Tabora ni moja ya Halmashauri nane za Mkoa wa Tabora ambazo zote ziko kwenye utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023, ambapo Mkoa wa Tabora pekee una madarasa 565. Manispaa ya Tabora ambayo inajenga madarasa 69, imeongoza katika kasi ya ujenzi wa madarasa hayo katika Mkoa wa Tabora.
Taarifa hii imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki katika majumuisho ya Ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Tabora yaliyofanyika Ziba, Wilaya ya Igunga, ambapo amekagua ubora na kasi ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023, lakini pia amekagua Shule zilizojengwa kwa fedha za mradi wa SEQUIP ambapo shule hizo nazo zinatarajia kupokea wanafunzi mwaka ujao wa 2023.
Waziri Kairuki amesisitiza Viongozi wote kwa nafasi zao waendelee kufuatilia miradi hii kwa ukaribu sana na akasisitiza kasi ya ujenzi wa madarasa haya iongezeke ili kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha mpaka kufikia Desemba 15, mwaka huu ujenzi uwe umekamilika.
Aidha Mhe. Kairuki amesisitiza taratibu za manunuzi ya Umma zifuatwe katika manunuzi yote ya bidhaa za ujenzi wa madarasa haya pamoja na miradi mingine yote ya Serikali. Waziri amesisitiza uaminifu sana na kuepuka asilimia kumi kwa wazabuni kwani vitendo hivi vya kifisadi vinazorotesha kuanzia ubora wa miradi mpaka kasi ya utekelezaji.
Mhe. Kairuki amewaonya Wafanyabiashara wanaoficha bidhaa za ujenzi ili ziadimike na kupandisha bei ya bidhaa hizo mathalani simenti na nondo, kwamba huo ni uhujumu uchumi na ameagiza Vyombo vya Dola viendelee kufuatilia watu hao na hatua za kisheria zichukuliwe pindi wanapobainika.
Wakati huohuo Mhe. Kairuki amewaomba Wananchi waendelee kuweka mchango wao mathalani nguvu kazi katika ujenzi wa miradi ya Serikali ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa ubora uliokusudiwa kwani maeneo mengi Nchi hii yanatofautiana na hivyo kuna baadhi ya maeneo fedha zinakuwa hazikidhi mahitaji, hivyo nguvu ya Wananchi inapoongezeka miradi hukamilika kwa ubora wake.
Katika maelekezo yake wakati wa majumuisho haya, Mhe.Waziri amewataka Wakurugenzi wawajengee uwezo ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kozi za muda mfupi mafundi wanaojenga miradi ya Serikali kwa mfumo wa Force Account, kwani mafundi hawa hususani ambao wanafanya vizuri kuna haja ya kuwapa mafunzo ili waendelee kufanya vizuri Zaidi.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.