Na Alex E. Siriyako;
Maelekezo haya ya Serikali yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda S. Buriani leo Novemba 24, akizindua Kampeni ya upandaji miti katika Mkoa wa Tabora, uzinduzi ambao umefanyika katika kijiji cha Igombe, Kata ya Kabila, Manispaa ya Tabora.
Uzinduzi huu wa Kimkoa unafuata baada ya Uzinduzi wa Kitaifa ambapo kila Mkoa ulipewa Malengo ambayo vilevile yalivunjwavunjwa hadi kufikia hatua ya Halmashauri ambapo kila Halmashauri inatakiwa kupanda miti isiyopungua milioni moja na laki tano kwa mwaka.
Katika uzinduzi huu ambao umeratibiwa na Tanzania Forest Services (TFS), taasisi za Umma na mashirika yasiyo ya Kiserikali nayo yameshiriki mathalani mabenki, TANESCO, Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Manispaa ya Tabora, pamoja na wadau wengine wa mazingira wakiwamo Wananchi wa Kata ya Kabila.
Mkuu wa Mkoa katika hotuba yake amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya ya kuleta fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo lakini pia kwa jitihada zake za makusudi za kupambana na changamoto na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha kwamba gesi ya kupikia majumbani inapatikana kwa bei ya chini sana kiasi cha kumfanya mwananchi wa kawaida asiwe na ulazima wa kutumia mkaa na kuni, kwani kwa hatua hiyo tutapunguza mahitaji ya mkaa hususani mijini na tutalinda misitu yetu.
Aidha katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kuwataka Wanachi wa Vijiji vya Ukumbi Kakonko na Usinga vilivyopo katika hifadhi ya mto Igombe katika Wilaya ya Kaliu waondoke kwa hiari mapema iwezekanavyo kabla Serikali haijaamua kutumia nguvu kuwatoa katika maeneo hayo. Na kwa msisitizo Dkt. Batilda ametanabaisha kuwa shughuli za kilimo zinaruhusiwa kufanyika kuanzia mita 300 kutoka chanzo cha maji hususani kwa wale wanaopakana na vyanzo vya maji.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Batilda amewataka Mamlaka ya kuhifadhi Misitu Tanzania (TFS) kwenda kwenye vyombo vya habari kuelimisha Umma wa Watanzania kuhusu sharia dhidi ya ukataji miti kiholela, sharia za Kudhibiti uharibifu wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kueleza adhabu anazoweza kukabiliana nazo mtuhumiwa pindi akikamatwa na vyombo vya usalama.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela amepata fursa ya kutoa salamu kwa hadhara hiyo, ambapo amemshuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia S. Hassan kwa fedha vyingi sana za miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Tabora hususani sekta ya Elimu, Afya na Barabara.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.