Na Alex Siriyako:
Kikundi -kazi cha Utekelezaji wa Mradi wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness Project ( TACTIC) kimemuelekeza Mkandarasi Chongqing International Construction Corporation ( CICO) kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu awamu ya kwanza katika Manispaa ya Tabora.
Maelekezo haya sambamba na maelekezo na ushauri mwingine wa kitaalamu yametolewa leo hii Machi 5,2023 ambapo wataalamu hawa kutoka Benki ya Dunia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI wametembelea barabara zote za mradi huu wa TACTIC awamu ya kwanza kwa Manispaa ya Tabora ambazo ni Kanyenye I, II & III( 1.99 km),barabara ya Swetu ( 1.99 km), barabara ya maili tano I,II, & III( 2.4 km), barabara ya Kisarika I, II, III( 2.9 km) pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mkandarasi.
Aidha Wataalamu hawa wameshauri kuangalia upya usanifu wa barabara ya Kisarika kutokana na sehemu kubwa ya barabara hii kuwa katika eneo linalokusanya maji mengi, lengo kuu likiwa ni ujenzi wa barabara hii usigeuke kuwa adha kwa Makazi yaliyo karibu na barabara hii mathalani kipande kilichopo karibu na Hospitali ya Malolo.
Vilevile Wataalamu hawa wameshauri Mkandarasi , Mhandisi Mkazi pamoja na Manispaa ya Tabora kushirikiana kuweka taratibu zote sawa ili watoa huduma kwa umma ambao huduma zao zinapita barabarani kama TANESCO, TUWASA pamoja na TTCL wanahamisha huduma hizo ili kupisha ujenzi wa barabara kwa wakati.
Zaidi ya yote, timu hii ya Wataalamu ikiongozwa na Mhandisi Erick Mwindi kwa upande wa Benki ya Dunia na Mhandisi Arif Almas kwa upande wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wamemsisitiza Mkandarasi kuwa eneo la Manispaa ya Tabora kwa ujumla wake kiwango cha maji kutoka ardhini ( Water Table) kiko juu sana, hivyo azingatie sana hilo katika ujenzi wa babara hizi.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.