Na Alex Siriyako,
Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Tabora imekutana leo hii katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora na kujadili namna bora ya kuhakikisha Chanjo ya Polio inawafikia walengwa ambao ni watoto walio chini ya miaka mitano kwa awamu hii ambayo ni awamu ya tatu.Hii ikiwa ni utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Utoaji wa Chanjo ya Matone ya Polio awamu ya tatu na zoezi hili litaanza mnamo tarehe 1/9/2022 hadi 4/9/2022.
Kikao cha kamati ya afya ya Msingi kimehudhuriwa na Wajumbe mbalimbali akiwemo mwenyekiti wa Kikao ambae ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora, Bi.Haika Masue akimwakilisha Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Paul Chacha, Mhe. Ramadhani Kapera,Mustahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Ndg.Nyahori Mahumbwe,Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Viongozi wa Dini mbalimbali,Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Wajumbe wengine wakiwemo Wataalamu wa Afya.
Polio ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Polio, ambacho huenezwa kwa kula chakula na kunywa maji yaliyo chafuliwa na kinyesi cha mtu mwenye ugonjwa huu. Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu kwa kutokuzingatia kanuni za usafi.
Dalili kuu za ugonjwa wa Polio ni Homa, Mafua, Maumivu ya mwili,kichwa na Shingo pamoja na Ulemavu wa ghafla wa Viungo. Watu walioko hatarini Zaidi kupata Polio ni Watoto chini ya miaka mitano(5), ingawa unaweza kuwapata watu wa rika zote.
Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kupata chanjo ya kukinga Polio. Na njia zingine ni kuzingatia usafi wa mikono pamoja na usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya Choo Bora. Miongoni mwa madhara makubwa ya Ugonjwa huu ni ulemavu wa Kudumu.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi,Bi.Haika amewaasa Wajumbe wote wakawe mstari wa mbele kuelimisha na kuhamasha Umma wa WanaTabora juu ya Umuhimu wa Chanjo ya Polio na madhara ya kutokupata chanjo hii,ili jamii ione kwamba hii ni fursa adhimu katika kupambana na Ugonjwa huu.
Bi.Haika ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua hizi za makusudi kufuatia Mgonjwa wa Polio kutangazwa Nchini Malawa mnamo tarehe 17, Februari ,2022,hivyo kutokana na Mwingiliano wa Tanzania na Malawi , Nchi yetu iko kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi hayo na hivyo kulazimika kuchukua hatua madhubuti.
Aidha Bi.Haika ameeleza kuwa Manispaa ya Tabora imepokea dozi sitini na tatu elfu(63,000) za chanjo ya matone ya Polio na zimeshasambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya na ameongeza kuwa Kampeni hii imelenga kuwafikia watoto hamsini na mbili elfu na mia nne themanini na sita (52,486) wenye umri chini ya miaka mitano.
Mwisho kabisa katika majumuisho ya kikao ,Wajumbe waliazimia kwamba Mawakala wa Sensa ya Unwani na Makazi inayoendelea watumiwe kuelimisha Umma kuhusu Polio, Vilevile Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, na Taasisi mbalimbali wahusishwe kwa ukamilifu ili kuelimisha Umma na kuleta wepesi wa utekelezaji wa kampeni hii.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.