Na Alex Siriyako:
Kamati ya Kudumu ya Mipangomiji ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambae pia ni Diwani wa Kata ya Kitete Mhe. Musa James Kaholyo, imetembelea na kukagua baadhi ya taasisi zilizo chini ya Manispaa ya Tabora mathalani Shule ya Msingi Manoleo, Shule ya Msingi Uhuru, Shule ya Msingi Town School pamoja na Shule ya Msingi Usule.
Katika Ziara hii ambayo imefanyika leo Februari 19,2023, Kamati imetembelea mradi wa upandaji miti uliopo Shule ya Msingi Manoleo Kata ya Itonjanda, Kamati imetembelea na kujionea hali halisi ya vyoo vilivyotitia kutokana na Mvua nyingi katika shule ya Msingi Uhuru iliyopo Kata ya Cheyo, Kamati imeona na kukagua madawati yaliyotengenezwa kwa mapato ya ndani, lakini pia imeshuhudia hali mbaya sana ya vyoo vilivyotitia na sehemu ya vyoo kubomoka katika shule ya Msingi Town School iliyopo Kata ya Gongoni. Aidha kamati imemaliza ziara yake kwa kutembelea na kukagua ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya Msingi Usule iliyopo Kata ya Mbugani.
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani wa Kamati hii ya Mipangomiji, wameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kutafuta bajeti ya dharula kukabiliana na uharibifu wa miundombinu ya vyoo iliyoharibika kutokana na Mnvua nyingi zinazoendelea kunyesha na kuongeza kuwa watoto hawawezi kusoma bila miundombinu hiyo muhimu na ya lazima.
Halikadhalika, Mwenyekiti wa Kamati hii amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi anazoipatia Manispaa ya Tabora, vilevile kwa niaba ya Kamati ameipongeza Manispaa ya Tabora kwa jitihada za makusudi na za vitendo za kuendelea kupambana na tatizo la upungufu wa madawati hasa katika shule za msingi katika Manispaa ya Tabora.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.