Na Alex Siriako:
Kamati ya Kudumu ya Fedha na Utawala imeeleza kuridhishwa na ubora wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika hatua tofauti tofauti katika Manispaa ya Tabora.
Wajumbe wa Kamati hii wameeleza haya leo Februari 23,2024 katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Katika ziara hii, Wajumbe wametembelea na kukagua ujenzi wa madarasa tisa katika shule ya msingi mabatini, ujenzi wa mabweni mawili, madarasa manne na ofisi nane, ujenzi wa uzio pamoja na ujenzi wa mfumo wa maji safi na maji taka katika shule ya sekondari Kazima, ukarabati wa Ofisi ya Kata ya Gongoni, pamoja na ujenzi wa madarasa matano, matundu nane ya vyoo katika shule ya sekondari Itonjanda.
Aidha, pamoja na kuridhishwa na ubora wa miradi hii ambayo kimsingi ipo katika hatua tofauti tofauti ya utekelezaji, wajumbe wameshauri fedha ambayo haijatumika katika ukarabati wa jengo la Utawala Kata ya Gongoni itolewe ili kukamilisha kabisa ukarabati huo na jengo lianze kutumika, pia wajumbe wameshauri uongozi wa shule ya sekondari Itonjanda kuongeza jitihada za kuwapata wazabuni ili utekelezaji wa mradi uendelee haraka kadri itakavyowezekana.
Mhe.Rose Kilimba, Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora ambae pia ni Diwani wa Kata ya Ifucha, kwa niaba ya Kamati ameishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia fedha za miradi ya maendeleo Manispaa ya Tabora.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.