Na Alex Siriyako;
Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kutatua kero mbalimbali za watumishi ndani ya Manispaa ya Tabora na Nchi nzima kwa ujumla. Baraza la Wafanyakazi limetoa pongezi hizi leo katika kikao maalumu cha kujadili na kupitisha Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mwenyekiti wa kikao ambae pia ni Mkurugenzi wa Halmashuri ya Manispaa ya Tabora Dr. Peter M. Nyanja amefungua kikao na kuwakaribisha wajumbe wote waliohudhuria kwenye mjadala huo. Miongoni mwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliohudhuria ni pamoja na Bw. Emmanuel Manzilili, Makamu Mwenyekiti TUKTA Mkoa wa Tabora, Bi. Digna Nyaki, Katibu C.W.T Mkoa wa Tabora, Dr. Charles Milambo, Mwenyekiti TUGHE Mkoa wa Tabora, Bw. Sareh Suleimani, Mwenyekiti TALGWU Mkoa wa Tabora, Wajumbe wa Baraza pamoja na Wataalamu wa Idara na Vitengo mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Pamoja na kumpongeza Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi na Wajumbe kwa pamoja wanamuomba sana Rais Samia kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora,aweze kuongeza jitihada za kuwapatia Watumishi haki na Stahiki zao ikiwemo upandaji wa madaraja kwa wakati, Wastaafu kupata fedha zao za kiinua mgongo kwa wakati, malipo ya mapunjo ya mishahara kwa watumishi, pamoja malipo ya fedha za likizo kwa watumishi na wastaafu yafanyike kwa wakati.
Mwenyekiti wa C.W.T Mkoa wa Tabora ambae vilevile ni Makamu Mwenyekiti wa TUKTA Mkoa wa Tabora, Bw. Emmanueli Manzilili kwaniaba ya wajumbe amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kwa kuimarisha Mshikamano na upendo wa Watumishi,pia amempongeza kwa jitihada zake za dhati za kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo hususani ngazi ya kata kwani mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imeshapeleka zaidi ya 26% kwenye miradi ya maendeleo kutoka mapato ya ndani.
Dr. Peter Nyanya ambae ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora na Mwenyekiti wa Baraza, katika kuhitimisha kikao amewapongeza Wajumbe kwa michango yao mizuri na ameahidi kupambania maslahi ya watumishi wa Halmashauri yake, amesisitiza kuwa ataendelea kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ngazi za chini kabisa kwa Wananchi na kupitia Baraza hili ameahidi kwamba Hospitalli ya Wilaya atahakikisha inafunguliwa Januari 15, 2022 ili kuwapa fursa Wananchi kupata huduma bora na kwa wakati.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.