Na Paul Kasembo - TMC.
Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Tabora kwa kauli moja limepisha Rasimu ya Bajeti ya Tzs Bilioni 48,921,386,574.89 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya wajumbe wa baraza pamoja na wataalamu wa Manispaa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja alisema kuwa Manispaa ya Tabora imekadiria kukusanya, kupokea na kutumia kiasi tajwa hapo juu kwa ajili ya mishahara, matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tumekusudia kufikia kiwango hicho ikiwa ni pamoja na ongezeko la Tzs 366,642.73 ambayo ni sawa na asilimia 6.8 ukilinganisha na bajeti ya 2021/2022 na ongezeko hili limetokana na kukasimia vyanzo vipya vya mapato kwa fedha za miradi ya maendeleo kupitia Ruzuku ya Serikali za Mitaa (LGCDG)” alisema Dkt. Nyanja.
Dkt. Nyanja alisema kuwa, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri imekusudia kuongeza mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vitano (5) vyenye uhakika na kuimarisha udhibiti wa ukusanyaji wa mapato hadi kufikia asilimia 100.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela alimpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu kwa namna ambavyo ameipatia fedha nyingi Manispaa ya Tabora kwenye bajeti yake kwa asilimia 98 haijawahi kutokea.
Mstahiki Meya pia limpongeza sana Mhe. Rais Samia Suluhu kwa kuipatia Manispaa ya Tabora fedha nyingi za UVIKO-19 ambazo zimewezesha kujenga Vyumba vya Madarasa na Ofisi za waalimu kwa Shule za Sekondari na Shule za Msingi na kukamilika tayari na wanafunzi wameanza kuyatumia tangu tarehe 17/1/2022 shule zilipofunguliwa.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu kwa namna ambavyo ameipatia fedha nyingi Manispaa ya Tabora ukianzia kwenye bajeti yenyewe tumepata asilimia 98 jambao ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa Manispaa hii, na kwa fedha za UVIKO-19, na sisi Manispaa ya Tabora tunamuahidi nidhamu kubwa zsana kwenye matumizi ya fedha hzio na ushirikiano wa kutosha tutampatia mama yetu”, alisema Mhe. Kapela.
Aidha aliwapongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Burian na viongozi wote wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda na viongozi wote ngazi ya Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja, Menejimenti, Watendaji wote pamoja na wadau kwa usimamizi na ufuatiliaji wao wa karibu kwenye miradi hii ambapo sasa tumefikia wakati tunajivunia mafanikio hayo yatokanayo ushirikiano wao.
Kando nao, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mhe. Mohamed Katete pamoja na kuwapongeza Mstahiki Meya wa Manispaa, Waheshimiwa Madiwani, Menejimenti na watumishi wote, lakini pia aliwakumbusha kwenda kusimamia maazimio yote yaliyofikiwa kwenye Baraza ili Manispaa iweze kufikia malengo kama inavyotarajiwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2022/2023 inakadiria kukusanya Tzs 5,451,254,158.28 kwa makusanyo ya vyanzo vya mapato ya ndani.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.