Na Alex Siriako:
Baraza la Madiwani la Manispaa ya Tabora kwa pamoja limetoa tamko la kumpongeza na kumshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia S. Hassan kwa kuipatia Manispaa ya Tabora kiasi cha Tsh.1,893,900,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vyoo pamoja na Shule mpya kabisa za Msingi.
Baraza limetoa tamko hili la pongezi na Shukrani leo Mei 12, 2023 katika kikao chake cha Baraza cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Fedha za Mradi wa BOOST kwa Manispaa ya Tabora zinajenga vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule za Chemchem ( madarasa 2), Izenga (madarasa 4 na matundu 3 ya vyoo), Kalunde (madarasa 3 na matundu 3 ya vyoo), Kizigo (madarasa 2 na matundu 3 ya vyoo) pamoja na Majengo (madarasa 3 na matundu 3 ya vyoo). Lakini pia fedha hizi zinajenga Shule mpya za Miyemba(mikondo 2), Magereza(mikondo 2) pamoja na Mabatini (mkondo 1).
Pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa, Baraza limejadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta zote zilizopo chini ya Halmashauri na kuridhika na kasi ya utekelezaji wa miradi,ikisimamiwa na timu ya Wataalamu wa Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mkurugenzi wao Dkt. Peter M. Nyanja.
Vilevile Madiwani wameelekeza Halmashauri kupitia Idara ya Mipangomiji ifanye uhakiki wa maeneo yake yote ili yawekwe kwenye mpango wa kuyaendeleza.
Baraza limepokea taarifa ya mapendekezo ya kujenga mabanda ya maduka katika eneo la mjini kati, nyuma ya standi mpya ambapo ndipo wafanyabiashara waliokuwa soko kuu wanapaswa kuhamia na wengine walishahamia tayari. Soko kuu la Mji wa Tabora inatarajiwa kujengwa kisasa kabisa kupitia mradi wa TACTIC. Baraza limepokea na kubariki mapendekezo hayo na kuongeza kuwa utekelezaji ufanyike haraka inavyowezekana.
Aidha Mhe. Ramadhani Kapela, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muunngano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia Manispaa ya Tabora fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo na akaongeza kuwa Manispaa ya Tabora ndani ya miaka miwili imetekeleza miradi mingi sana hususani kwenye sekta ya Afya, Elimu na Kilimo kwa Zaidi ya asilimia mia moja ya Bajeti, kitu ambacho toka uhuru hakijawahi kutokea.
Katika kuhitimisha kikao cha Baraza hili, Bi.Neema Kapesa, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, amewashukuru wajumbe wa Baraza na kuahidi kuwa atatekeleza maelekezo waliyotoa na amepokea ushauri wao kwa heshima kubwa kabisa. Aidha Bi.Neema nae amemshukuru Mhe.Rais kwa kuendelea kuipa upendeleo Manispaa ya Tabora hususani kwenye miradi ya kimkakati.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.