Na Alex Siriyako;
Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania tawi la Mkoa wa Tabora imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika manispaa ya Tabora leo Januari 14,2023. Jumuiya hii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Diwani Adam H. Malunkwi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo imekagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Taboara.
Wajumbe wa ALAT wakiwamo Wabunge, Madiwani pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri nane(8) za Mkoa wa Tabora wamepata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya, Elimu pamoja na Utawala. Miradi hiyo ni Jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Hospitali Mpya ya Manispaa ya Tabora ambayo imeshaanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje(OPD), Shule ya Sekondari Uledi ambayo ni shule mpya na ipo kata ya Mpera na imeshaanza kupokea wanafunzi mwaka huu, Ujenzi wa Madarasa manne na Ofisi mbili shule ya Msingi Bombamzinga pamoja na Kiwanja cha uwekezaji kinachomilikiwa na ALAT Mkoa wa Tabora.
Aidha katika majumuisho ya ziara ya kukagua miradi hii ya maendeleo, wajumbe wamefurahishwa sana na ubora wa miradi husika na kuongeza kuwa thamani ya pesa iliyotumika inaonekana na vilevile wamewashukuru mafundi ujenzi kwa kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa kwani pesa za Serikali muda mwingine zinakuwa hazitoshi mahitaji na ni lazima mradi husika ukamilike kwa fedha zilizopatikana.
Lakini vilevile Wajumbe wametoa ushauri na nasaha zao kwa Menejimenti ya Manispaa ya Tabora inayoongozwa na Mkurugenzi wake Dkt. Peter M. Nyanja kuwa mradi kama wa Jengo la Utawala ni wa Jengo la ghorofa na ni bora bajeti ya kuweka LIFTI(Elevator) ikaanza kutafutwa kwani jingo hilo kwa uzuri wake halifai kukaa bila LIFTI. Wajumbe wameongeza kuwa Mkurugenzi atafute fedha aweze kumalizia madarasa mawili na ofisi moja ambayo yameanzishwa kwa nguvu za Wananchi wa kata ya Isevya.
Kwa kuhitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tabora Mhe. Adam Malunkwi amewasihi wajumbe katika maeneo yao wajitahidi kukemea tabia za baadhi ya watu ambao kwa nia isiyokuwa njema wanafanya kazi ya kuzichafua Halmashauri za Mkoa wa Tabora, Chama cha Mapinduzi na Serikali kwa Ujumla, na kwa pamoja Wajumbe wameahidi kulifanyia kazi suala hili.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.